Jimbo Katoliki Kitui, Kenya linasherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake!
Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Jumamosi tarehe 16
Agosti 2014 ameiongoza Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya kumwimbia
Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu
Jimbo hili lilipoanzishwa na Mapadre wa Roho Mtakatifu. Kardinali Njue amewataka waamini
Jimboni humo kujifunga kibwebwe ili kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji ulioanzishwa
na Wamissionari Jimboni humo!
Kardinali Njue amewaambia waamini kwamba, Wamissionari
walipandikiza mbegu ya Ukristo, wakiwa na nia ya kutaka kuhakikisha kwamba, Habari
Njema ya Wokovu inawafikia pia wananchi wa Kitui. Maadhimisho haya ni fursa makini
ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuangalia ikiwa kama kweli ile mbegu ya Ukristo iliyopandwa
na Wamissionari imekuwa na kuzaa matunda ya toba, wongofu na utakatifu wa maisha.
Ibada hii imehudhuriwa na idadi kubwa ya Maaskofu kutoka Kenya pamoja na kupata
baraka ya uwepo wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Rais Kenyatta amelipongeza Kanisa
Katoliki kwa kazi kubwa ambalo limewafanyia wananchi wa Kenya katika kipindi cha miaka
50 iliyopita. Waamini wamepata chakula cha maisha ya kiroho, lakini pia Kanisa limeisaidia
Serikali kutekeleza barabara wajibu na dhamana yake kwa wananchi wa Kenya, hususan
katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima:
kiroho na kimwili.
Kanisa nchini Kenya limechanfia kwa kiasi kikubwa katika
maboresho ya maisha ya wananchi wa Kenya, changamoto kwa Serikali na Kanisa kuendelea
kushirikiana katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo kwa wananchi wa Kenya.
Katika
tukio hili, Askofu Anthony Muheria wa Jimbo la Kitui, ameadhimisha Kumbu kumbu ya
miaka 10 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Embu, ambako aliwahudumia
watu wa Mungu kwa miaka minne na baadaye akateuliwa kuongoza Jimbo Katoliki la Kitui
na tayari miaka sita imekwisha yoyoma. Jimbo Katoliki la Kitui lilimegwa kutoka Jimbo
kuu la Nairobi kunako mwaka 1956 na Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI na kunako mwaka
1963 Monsinyo William Dunne, akateuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la
Kitui. Jimbo hili limewahi kuhudumiwa na Marehemu Askofu mkuu Bonoface Lele kabla
ya kukabidhiwa kwa Askofu Muheria.
Jimbo Katoliki la Kitui linatoa huduma za
kichungaji katika elimu, afya na maendeleo endelevu, huduma inayosimamiwa na Shirika
la Misaada la Kanisa Katoliki Kenya, Caritas Kenya.