Mchakato wa majadiliano kati ya Kanisa na walimwengu!
Kanisa linalojikita katika majadiliano ya kina: Mapitio ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa
Vatican, ndiyo kauli mbiu itakayoongoza Kongamano la kitaifa la siku mbili litakalofanyika
nchini Ubelgiji kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 28 Oktoba 2014. Kati ya washiriki wakuu
wa Kongamano hili ni pamoja na Kardinali Gerhard Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa
la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.
Itakumbukwa
kwamba, maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yalifanyika kuanzia mwaka 1962
hadi mwaka 1965 na hapa ukawa ni mwanzo wa Kanisa linalojadili mintarafu Ufunuo wa
Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee majadiliano ya kidini na kiekumene na waamini
wa dini mbali mbali pamoja na tamaduni zilizoko katika ulimwengu mamboleo.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Ubelgiji linasema kwamba, majadiliano ya kidini na kiekumene
yanafumbatwa katika misingi ya ukweli, uwazi, upendo na mshikamano wa dhati. Ni mchakato
wa kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kwa mwelekeo huu, Familia ya Mungu nchini Ubelgiji itajadili kuhusu: nyaraka za Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na: majadiliano ya kidini na kiekumene;
Utangazaji wa Habari Njema kwa Watu wa Mataifa, Kanisa katika Ulimwengu pamoja na
kuangalia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mapambazuko ya Millenia ya tatu
ya Ukristo, zinazohitaji mikakati ya Uinjilishaji Mpya kama anavyofafanua kwa kina
Baba Mtakatifu Francisko.
Maadhimisho ya Kongamano hili yatafanyika kwa kipindi
cha siku tatu, katika maeneo matatu tofauti, ili kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu
katika tukio hili la kihistoria. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi, itaadhimishwa
kwenye Kanisa kuu la Koelberg mjini Brussels na Askofu mkuu Andrè-Joseph Leonard.
Wajumbe wa kongamano hili pamoja na mambo mengine watapembua kwa kina na mapana tema
kuhusu “Utamadunisho na Ugunduzi” mahusiano yaliyopo kati ya Mapokeo ya Kikristo na
utamaduni mamboleo.