Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika
ya Kati, katika mahubiri yake wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu hivi
karibuni, amewataka viongozi wa Serikali na wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanafanya
maamuzi magumu ili kuokoa maisha ya watu na mali zao Nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika
ya Kati.
Askofu mkuu Nzapalainga kwa niaba ya wakimbizi na watu wasiokuwa
na makazi maalum nchini humo, amemwomba Waziri mkuu mpya Mahamat Kamoun, kufanya
maamuzi magumu, ili kuokoa maisha ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana na machafuko
ya kisiasa nchini humo. Bado watu wanauwawa kikatili licha ya Kikundi cha Seleka na
Wanajeshi wa Balaka kutiliana sahihi mkataba wa kusitisha mapigano hapo tarehe 23
Julai 2014 mjini Brazzaville.
Tarehe 14 Agosti 2014 Waziri mkuu Mahamat Kamoun,
aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais Samba Panza aliapishwa rasmi na kuanza kutekeleza
majukumu yake kama Waziri mkuu wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.