2014-08-19 08:39:55

Sinodi za majimbo nchini Burundi zinapania kujenga, kuimarisha na kudumisha umoja wa kitaifa, ili kukoleza imani, matumaini na mapendo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi limejiwekea mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa kuadhimisha Sinodi za Majimbo ili kujenga, kuimarisha na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kukoleza imani, matumaini na mapendo kati ya watu. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu Gervais Banshimiyubusa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi. RealAudioMP3

Kwa njia ya maadhimisho ya Sinodi za Majimbo, Maaskofu wanapania kuona kwamba, waamini wanaifahamu imani wanayoiungama katika Kanuni ya Imani, Imani wanayoiadhimisha katika Sakramenti na Liturujia ya Kanisa; Imani wanayoimwilisha katika matendo adili, wakiongozwa na Amri za Mungu na Imani wanayoisali na kuitekeleza kwa vitendo katika matendo ya huruma. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anashiriki kikamilifu katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linasema, kati ya zawadi kubwa waliyopewa na Roho Mtakatifu katika siku za hivi karibuni ni kukamilika kwa tafsiri ya Biblia Takatifu kwa lugha ya Kirundi, ambayo ni lugha ya taifa nchini humo. Biblia hii itawasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuweza kusoma, kutafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Kanisa Katoliki nchini Burundi linaendelea kukua na kupanuka, kwani hivi karibuni kumeanzishwa Seminari kuu na hivyo kulifanya Kanisa Katoliki Burundi kuwa na Seminari kuu nne, dalili za kuongeza kwa miito ya Upadre na Utawa. Kwa sasa Maaskofu wanapenda kujielekeza zaidi katika majiundo makini ya Majandokasisi: kiakili, kiutu, kiroho na katika shughuli za kichungaji, ili Mapadre wanaotoka Seminarini humo waweze kuwa wamefundwa na kuiva barabara tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Maaskofu wanaishukuru Familia ya Mungu nchini Burundi ambayo inaendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Hili pia ni jambo la kumshukuru Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu katoliki Burundi wakati wa hija yao ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano aliwataka kujielekeza kwa namna ya pekee katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Burundi. Alimkumbuka kwa namna ya pekee Marehemu Askofu mkuu Michael A. Courtney aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi aliyeuwawa kikatili na watu wasiojulikana kunako tarehe 29 Desemba 2003. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai, mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake katika utekelezaji wa utume wake nchini Burundi.

Baba Mtakatifu Francisko aliwapongeza Maaskofu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya ili waweze kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Burundi inayojikita katika haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa!








All the contents on this site are copyrighted ©.