2014-08-19 08:59:53

Msaada kwa wananchi wa Iraq kutoka Cor Unum


Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum katika taarifa yake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameguswa sana na mahangaiko pamoja na mateso ya wananchi wa Iraq na mara kwa mara ameendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho. Itakumbukwa kwamba, amemtuma Kardinali Fernando Filoni, kama mjumbe wake maalum nchini Iraq ili kuonesha mshikamano wake wa upendo.

Cor Unum linasema, tangu Mwezi Juni, Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Iraq yamekuwa mstari wa mbele kutoa msaada kwa wakimbizi na wahamiaji. Hadi sasa zaidi ya familia 4, 000 zimekwishasaidiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Iraq pamoja na mashirika mengine ya misaada ya Kanisa Katoliki, huduma inayoratibiwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwasaidia wananchi wa Iraq si tu kwa njia ya sala na sadaka yake, bali pia kwa njia ya rasilimali fedha, ili kuwasaidia wananchi wa Iraq kupata mahitaji msingi katika kipindi hiki kigumu. Cor Unum inaendelea kushirikiana kwa karibu sana na viongozi wa Makanisa ya Mashariki nchini Iraq.

Msaada unaotolewa na Kanisa Katoliki unalenga zaidi katika kuwapatia wananchi msaada wa chakula, huduma ya afya na elimu kwa watoto na vijana. Cor Unum inasema inaendelea kufanya upembuzi yakinifu katika eneo la tukio ili kubainisha mahitaji muhimu yatakayofanyiwa kazi kwa siku za usoni!







All the contents on this site are copyrighted ©.