Baba Mtakatifu Francisko amewasha moto nchini Korea!
Askofu Peter Kang U-il, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini anasema,
hija ya Baba Mtakatifu nchini mwao imekuwa na mafanikio makubwa katika maisha ya watu
kiimani na imeacha chapa na alama ya kudumu kwa maisha ya waamini na wananchi wa Korea
katika ujumla wao. Hili ni tukio ambalo limefuatiliwa kwa umakini mkubwa na vyombo
vya habari ndani na nje ya Korea.
Askofu Peter anasema, kwake, kilele cha hija
ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea kilikuwa pale alipowatembelea watoto wenye
mtindio wa ubongo, akawakumbatia, akawafriji na kuwabariki. Hawa ni watoto wanaoishi
katika mazingira magumu na hatarishi, ni watoto walitelekezwa na wazazi wao kutokana
na ulemavu, ni watoto waliokuwa wanachungulia kaburi, lakini wameonja upendo mkuu
kutoka kwa Mama Kanisa.
Baba Mtakatifu alitumia muda mrefu kumsalimia kila
mtoto, tukio lililopelekea kusitishwa kwa Sala ya Masifu ya Jioni kati ya Baba Mtakatifu
na Watawa. Lakini Baba Mtakatifu mwenyewe aliwaambia kwamba, Sala ni muhimu sana katika
maisha ya waamini, lakini huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii ina umuhimu wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani hii ni sala inayomwilishwa
katika matendo!
Baba Mtakatifu alipenda kukazia umuhimu wa Kanisa kushikamana
na maskini, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Huu ndio ujumbe muhimu sana
kwa waamini na wananchi wa Korea katika ujumla wao, Kanisa halina budi kujitambulisha
na kuwahudumia maskini!
Askofu Peter anasema, Baba Mtakatifu amewaachia wananchi
wa Korea shauku kubwa katika maisha yao kutokana na unyenyekevu pamoja na kuguswa
na maisha ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Tukio la kuwatangaza
Mashahidi na wafiadini wa Korea kuwa ni Wenyeheri. Hii ni changamoto kubwa kwa waamini
nchini Korea kuendelea kuonesha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda
wa maisha na imani inayomwilishwa katika matendo.
Faraja iliyotolewa na Baba
Mtakatifu kwa watu walioguswa na ajali ya kuzama kwa Meli Sewol, imewapatia wananchi
wengi faraja baada ya kuondokewa na wapendwa wao. Baba Mtakatifu aliweza kuzungumza
na kuwapatia neno la faraja, kama mbegu ya kuponya madonda ya ndani, tayari kuanza
tena safari ya maisha, wakiwa na mwelekeo mpya.
Hapa Baba Mtakatifu aliguswa
na mahangaiko yao, akayashiriki kwa imani na matumaini. Hiki kilikuwa ni kielelezo
cha uwepo wa karibu katika hija yao ya maisha, inayohitaji kweli uponyaji wa ndani.
Watu hawa hawatasahau tukio hili katika maisha yao.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu
Francisko kwa vijana Barani Asia ni changamoto endelevu inayowataka vijana kusimama
imara katika misingi ya imani, maadili na utu wema. Amani na Upatanisho, Umoja wa
Kitaifa na Udugu ni mambo msingi ambayo wananchi wote wa Korea wanapaswa kuyafanyia
kazi, ili kuimarisha upendo na mshikamano wa kitaifa, wakiwa wanatembea kwa pamoja
kama ndugu wamoja!