Baba Mtakatifu Francisko katika siku yake ya mwisho nchini Korea, Jumatatu tarehe
18 Agosti 2014, ameanza kwa kukutana na kusalimiana na viongozi wa kidini nchini Korea
na baadaye ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho
nchini Korea, ibada ambayo imehudhuriwa pia na viongozi wa Serikali kutoka Korea ya
Kusini. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Meyong-dong la Jimbo kuu la Seoul,
Korea.
Baba Mtakatifu ameanza Ibada hii kwa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya
amani na upatanisho kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Korea. Liturujia ya Neno
la Mungu imejikita katika umoja unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
baada ya watu kutopea katika utengano na mgawanyiko. Mwenyezi Mungu anawapatia ahadi
ya kuwaunganisha tena, ikiwa kama wataheshimu na kutii amri zake kutoka katika undani
wa mioyo yao!
Baba Mtakatifu anasema upatanisho, umoja na amani ni zawadi kutoka
kwa Mwenyezi Mungu inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Hii ni changamoto
ya kufanya mabadiliko ya kweli kutoka katika undani wa moyo wa mwanadamu, hali inayoweza
kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na historia ya mtu binafsi na kama Jamii ya
watu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema mang'amuzi haya yanajidhihirisha kwa
namna ya pekee katika mazingira ya historia ya wananchi wa Korea; haya ni mang'amuzi
ya utengano na kinzani ambazo zimekuwepo kwa takribani miaka sabini. Mwenyezi Mungu
anawaalika waamini na wananchi wa Korea katika ujumla wao kutubu na kumwongokea; kufanya
tafakari ya kina kuhusu mchango wao katika ubora wa ujenzi wa Jamii inayojikita katika
haki na ubinadamu.
Wananchi wa Korea wanaalikwa kutafakari kama mtu binafsi
na Jumuiya, jinsi wanavyotolea ushuhuda wa Kiinjili kwa ajili ya maskini, watu wanaotengwa
na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii; kwa watu wasiokuwa na fursa za ajira au wale ambao
wametengwa kutoka kwenye mchakato wa maendeleo ya wengi. Mwenyezi Mungu anawaalika
kama Wakristo na kama wananchi wa Korea kuachana na mawazo ya kudhaniana vibaya, kinzani
na ushindani usiokuwa na tija wala mashiko.
Baba Mtakatifu Francisko katika
mahubiri yake anasema Yesu anawataka kuamini kwamba, msamaha ni mlango unaowaelekeza
watu katika upatanisho. Anawataka wafuasi wake kujikita katika upatanisho bila kubakiza
kinyongo. Anawataka kufanya mabadiliko ya kweli na anawajalia neema ya kutekeleza
kazi hii. Msalaba wa Kristo unaonesha ile nguvu ya Mwenyezi Mungu katika kutuliza
utengano, kuganga madonda na kujenga tena mahusiano yanayojikita katika upendo wa
kidugu.
Na kwa mawazo haya, Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake nchini
Korea, akiwataka waamini nchini Korea kuwa na imani katika nguvu ya Msalaba wa Kristo;
kujenga na kuimarisha ari na moyo wa urafiki kati ya Wakristo, waamini wa dini mbali
mbali pamoja na watu wenye mapenzi mema nchini humo, watu ambao wana taka kuona mafanikio
ya mustakabali wa Korea; kwani wao watakuwa ni chachu ya Ufalme wa Mungu nchini Korea.
Baba
Mtakatifu Francisko amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Korea
kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia fursa za majadiliano, mikutano
na moyo wa kutaka kuvuka vikwazo vya kutowajali wengine; bali kwa kuendeleza ukarimu
kwa kuwasaidia maskini pamoja na kutambua kwa mapana zaidi ukweli kwamba, wananchi
wote wa Korea ni ndugu na watu wa familia moja!
Wakati wa Sala ya Waamini,
Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka na kumwombea Kardinali Fernando Filoni ambaye
alipaswa kuwa kwenye msafara wa Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini
Korea, lakini akalazimika kwenda Iraq kumwakilisha, kama kielelezo cha mshikamano
wa dhati na watu wanaoteseka na kudhulumiwa nchini Iraq. Baba Mtakatifu anamwomba
Yesu Kristo ili aweze kuwa karibu naye katika maisha na utume wake huko Iraq.