2014-08-17 11:32:29

Zingatieni imani, kanuni maadili na utu wema!


Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, amdewataka wakuu wa shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Kenya kuhakikisha kwamba wanasaidia kuwarithisha vijana wa kizazi kipya tunu msingi za maisha ya Kikristo, maadili na utu wema.

Watambue kwamba, utoaji wa elimu ya dini shuleni ni dhamana na jukumu ambalo linapaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa, kwani ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, dhamana inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kardinali Njue anawataka waalimu na wadau wengine kujisadaka kweli kweli ili kuwarithisha vijana wa kizazi kipya tunu msingi za Kikristo, ili waweze kukabiliana vyema na changamoto za maisha ya ujana, huku wakiwa wamejikita katika kanuni maadili na utu wema.

Kardinali Njue anawataka walimu na wazazi kusimama kidete kupinga muswada wa sheria ya afya ya uzazi ya mwaka 2014 inayotaka kutoa ruhusa kwa Serikali kutoa vizuia mimba kwa watoto kuanzia umri wa miaka kumi, jambo ambalo anasema ni hatari kwa maadili na utu wema. Shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa hazitaruhusu kampeni hii kufanyika katika maeneo yao. Kuna haja ya kuweka uwiano bora kati ya imani na maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.