2014-08-17 11:44:31

Vijana simameni kidete kwani mna wajibu na dhamana!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 17 Agosti 2014, amehitimisha maadhimisho ya Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu "Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia" kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Boma la Haemi, lililojengwa kunako mwaka 1421 kama kinga dhidi ya maharamia na kunako mwaka 1490 boma hili likageuzwa kuwa ni kituo cha kijeshi.Tukio hili limehudhuriwa na vijana kutoka katika mataifa ishirini na mbili.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekiri kwamba, tema iliyochaguliwa na Maaskofu katika maadhimisho ya Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia inatoa mwelekeo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana. Huu ni ushuhuda mkubwa unaoungama imani kwa Kristo. Vijana Barani Asia, simameni, hii ni dhamana na wajibu ambao kweli vijana wanapaswa kuutekeleza katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, vijana kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Asia wamekusanyika nchini Korea. Bara la Asia lina utajiri mkubwa wa mapokeo, falsafa na dini na kwamba, huu ni uwanja ambao waamini wanapaswa kuutumia ili kushuhudia imani yao kwa Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima.

Vijana wanakumbushwa kwamba, wao ni watoto wa Bara la Asia, wana haki na dhamana ya kushiriki kikamilifu katika maisha ya jamii zao. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuondokana na woga ili kupeleka hekima ya imani katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii. Vijana waone na kupenda kile ambacho ni chema, kizuri na kweli kutoka katika tamaduni na mapokeo yao. Watambue kwamba, Injili ina nguvu ya kuweza kusafisha, kuinua na kukamilisha hazina hii kubwa.

Vijana wawe makini kung'amua kile ambacho ni kinyume cha imani ya Kanisa Katoliki, yaani mambo ambayo yanakwenda kinyume cha maisha ya neema iliyomiminwa mioyoni mwao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo; wawe waangalifu kwa tamaduni mamboleo zinazoweza kuwatumbukiza katika dhambi, rushwa na hatimaye, kuwasukumizia katika kifo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema ujana ni kielelezo cha matumaini makubwa, nguvu na utashi mwema, mambo yanayogubika maisha ya ujana. Vijana wanachangamotishwa na Mama Kanisa kumwachia nafasi Yesu, ili aweze kuwaletea mabadiliko yanayojikita katika matumaini ya Kikristo na nguvu zao katika fadhila za kimaadili; matashi yao mema yageuzwe katika upendo unaothubutu kujisadaka.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba wao ni matumaini ya Kanisa kwa siku za usoni na sehemu muhimu sana inayopendwa na Kanisa kwa wakati huu. Anawataka vijana kuendelea kuungana, ili kulijenga Kanisa ambalo ni takatifu zaidi, Kanisa la Kimissionari na linalojikita katika unyenyekevu; Kanisa ambalo linampenda na kumwabudu Mwenyezi Mungu; Kanisa linalojielekeza zaidi katika huduma kwa maskini, wapweke, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana kutoka Barani Asia, kusimama imara kama kielelezo cha dhamana ambayo wanakabidhiwa na Yesu mwenyewe. Wanatakiwa kuwa macho na makini, ili mashikinikizo, majaribu na dhambi zao au zile za jirani zao zisivuruge umakini wao kuhusu uzuri wa utakatifu wa maisha kwa ajili ya Furaha ya Injili.







All the contents on this site are copyrighted ©.