Mama wakuu wa Mashirika ya Kitawa kutoka katika nchi za AMECEA wameanza mkutano wao
mjini Lusaka
Shirikisho la Mabaraza ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki, ACWECA, Jumapili tarehe
17 Agosti 2014 limefungua mkutano wake wa kumi na sita Jimbo kuu la Lusaka, Zambia
kwa kuongozwa na kauli mbiu "Nenda, usiogope, kahudumie". Mkutano huu unawajumuisha
Mama wakuu wa Mashirika ya Kitawa 150 kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA.
Ni mkutano unaohudhuriwa pia na
viongozi wakuu wa AMECEA waliochaguliwa hivi karibuni katika mkutano wake uliofanyika
mjini Lilongwe, Malawi. Mkutano huu unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 30 Agosti
2014. Pamoja na mambo mengine, Mama wakuu wa Mashirika ya Kitawa kutoka katika nchi
za AMECEA wanajadili kuhusu: mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, Sheria
za Kanisa na Kiraia, Uwazi katika masuala ya uongozi; uwajibikaji; udhibiti wa fedha
za Kanisa pamoja na kuandaa bajeti ya Mashirika. Wajumbe pia watasilikiza taarifa
ya Shirikisho la Mama wakuu wa Mashirika ya Kitawa Afrika Mashariki na Kati.
Shirikisho
hili lilianzishwa kunako mwaka 1974 na kwa sasa linawajumuisha Watawa wa kike wapatao
20, 000. ACWECA pamoja na mambo mengine, linapania kukuza na kuendeleza majiundo makini
ya watawa; kuwajengea uwezo watawa ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato
wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani pamoja na kujitegemea. Ni Shirikisho
linalotoa msaada wa kiufundi kwa Mashirika ya Kitawa, ili kweli watawa waweze kuwa
ni Mashahidi wa Kristo kati ya watu wanaowahudumia katika sekta mbali mbali za maisha.