Bwana Lee Ho Jin abatizwa na kuimarishwa kwa Kipaimara na Papa Francisko mjini Seoul!
Baba Mtakatifu Francisko, ameianza siku ya Jumapili tarehe 17 Agosti 2014 kwa kuadhimisha
Ibada ambamo ametoa Sakramenti ya Ubatizo, kwa Bwana Lee Ho Jin kwenye Kikanisa cha
Ubalozi wa Vatican mjini Seoul, Korea ya Kusini. Huyu ni baba wa mtoto kati ya watoto
waliozama na kufa maji kwenye ajali ya Meli iliyotokea Sewol, Korea ya Kusini.
Bwana
Lee alionesha nia ya kutaka kubatizwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na waathirika
wa ajali ya Meli kwenye Uwanja wa Michezo Kimataifa mjini Daejeon. Bwana Lee alitembea
umbali wa kilometa tisini kwa mguu aklwa amebeba Msalaba ambao alimkabidhi Baba Mtakatifu
Francisko kama kielelezo cha maombolezo yake kutokana na msiba mkubwa uliokuwa umewafika.
Katika Ibada hii, Bwana Lee alikuwa ameongozana na watoto wake wawili na Msimamizi
wa Ubatizo alikuwa ni mwamini mlei kutoka Ubalozi wa Vatican nchini Korea.
Ibada
hii imeadhimishwa katika lugha ya Kikorea na Padre John Chong Che-chon, Myesuit ambaye
kwa sasa ni Mkarimani wa Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kichungaji nchini
Korea. Baba Mtakatifu amembatiza na baadaye kumwimarisha kwa Sakramenti ya Kipaimara
na amejichagulia jina la Francisko. Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican
anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu amefurahi kuweza kushiriki katika tukio hili la
kiimani ambalo halikuwa limepangwa katika hija yake, matendo makuu ya Mungu.