Wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu
kwa ajili ya Familia sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Familia kwa baadhi ya majimbo
nchini Tanzania, Ndugu Antipasi Shinyambala ana machache ya kuishirikisha Familia
ya Mungu katika kutambua wajibu wa wazazi kwa watoto wao.
Swali kuu, familia
zinaeleza nini kwa watoto? Je, wazazi wana muda wa kukaa, kusali na kula pamoja na
watoto wao? Je, wazazi wana muda wa kuwafundisha watoto wao wenyewe juu ya imani na
mafundisho tanzu ya Kanisa wanayosimamia na kujitahidi kuyaishi?
"Yesu
aliletewa watoto wadogo ili aweke mikono juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea.
Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana
waliomfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka
huko.." (Mt. 19:13-15).
Wanafunzi wa Yesu walitaka kuwazuia watoto wasiende
kumpotezea muda Yesu. Mitume walijua kuwa Yesu alikuwa ni kwa ajili ya watu wakubwa
tu. Lakini Yesu anatufundisha thamani ya kuwekeza kwa watoto wetu. Hata sisi mara
nyingi tunaingia katika mtego huu wa kuwaona watoto hawawezi kujua kitu juu ya ufalme
wa Mungu. Tukishawabatiza watoto wetu basi, labda tunaenda nao kanisani kama mazoea
tu hatuwafuatilii kama wanacheza au wanasali.
Ni utamaduni au mtindo wa familia
nyingi kuwa baada ya kuwabatiza watoto huwa tunawekeza juu ya elimu ya kidunia zaidi
na ya kimungu kama ziada. Hatuwekezi sana juu ya elimu ya Mungu hadi wakati wa mafundisho
ya komunyo na kipaimara, matokeo yake watoto wetu wanakuwakimwili lakini bila kuwa
na misingi bora ya dini. Biblia kwao ni shida wakati masomo ya kidunia, ambayo ni
magumu, wanafaulu vizuri sana.
Tunaona hayo ni sawa kwa kuwa hawataajiliwa
kwa kigezo cha kujua Biblia au mafundisho ya Mungu. Tunashindwa kuwajenga katika misingi
imara ya imani. Watoto wanakuja kusikia kuwa kulipa zaka ni amri, kujenga makanisa
ni wajibu wao, wakati wameshajua utamu wa fedha, lazima wajue tu mapadre wa siku hizi
wanapenda sana hela na si vinginevyo.
Tukijikita kuwawekea misingi mizuri
watoto wetu, wataifuata kwani watoto ni tegemezi, mioyo na akili ya watoto ina nafasi
kubwa sana kushika jambo lolote wanalofundishwa na wanaamini kuwa wanachoambiwa na
wazazi ni kila kitu. Kazi yetu kwa watoto ni kuamua kuwaunda watoto wetu tunavyotaka,
je, tunawapeleka wapi watoto wetu, tunawaruhusu Yesu awafundishe?
Tumuombe
Mungu atupe unyenyekevu wa kuwa na akili ya kupokea mafundisho na amri za Mungu kama
watoto wadogo, atupe hekima juu ya malezi ya watoto wetu. Tuwaombea watoto wetu ili
wakue katika misingi ya hofu ya Mungu ili wawe warithi bora wa imani yetu. Tumsifu
Yesu Kristu!