2014-08-16 10:33:19

Mashahidi wa Korea walitafuta ukweli, wakaonesha uaminifu wao kwa kanuni msingi, kielelezo cha upendo na mshikamano kati ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 16 Agosti 2014 amewatangaza Watumishi wa Mungu 124 kutoka Korea kuwa ni Wenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na maelfu ya waamini na watu wenye mapenzi mema kwenye lango kuu la Gwanhwamum, Jimboni Seoul. Hii ni mara ya tatu kwa Kanisa nchini Korea kuadhimisha Ibada ya watoto wake kutangazwa kuwa ni Wenyeheri. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kuhusu Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anasema hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kumtenga mwamini na upendo wa Kristo; si dhiki, shida, adha, njaa, hatari wala upanga. Hazina hii imekuwa ni sehemu ya utajiri ulioiwezesha Jamii ya Korea kuwa ni Kanisa la Kristo. Imani ya Kikristo haikuwafikia wananchi wa Korea kwa njia ya Wamissionari kama ilivyo katika sehemu nyingine za dunia, bali hapa imani imepenyeza katika mioyo na akili za watu. Ni watu waliochangamotishwa na udadisi wa kiakili na tafiti za kweli kuhusu maisha ya kidini. Baada ya kukutana na Injili, wananchi wa Korea wakafungua akili yao kwa Yesu.

Baba Mtakatifu anasema kwa njia hii wakabatizwa na kuanza kujikita katika ukamilifu wa maisha ya Kisakramenti na Kikanisa, na huo ukawa ni mwanzo wa ari na mwamko wa kimissionari. Ni Kanisa ambalo limetoa matunda yake kwa kufuata mfano wa Kanisa la Mwanzo, ambako waamini walikuwa ni roho na moyo mmoja, bila kuhangaikia tofauti za mapokeo na za kijamii na wakaweka mambo yote katika ushirika.

Baba Mtakatifu anasema, urithi wa Mwenyeheri Paulo Yun Ji-chung na wenzake, katika mchakato wa kutafuta ukweli wakionesha uaminifu wao kwa kanuni msingi za maisha ya kidini, walizoamua kuzizingatia, wakaonesha ushuhuda wa upendo na mshikamano kwa wote, kielelezo makini cha utajiri wa historia ya wananchi wa Korea.

Urithi wa Mashahidi wa Korea ni changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema katika utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa utulivu; haki, uhuru na upatanisho, mambo msingi katika ujenzi wa amani pamoja na ulinzi wa tunu msingi za maisha ya kiutu nchini Korea na Ulimwenguni kote.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anakazia kuhusu Injili, ambayo Yesu anamwomba Baba yake wa mbinguni kuwaimarisha wafuasi wake katika kutafuta ukweli pamoja na kuwalinda hapa duniani. Sala hii ni muhimu sana anasema Baba Mtakatifu, kwani Yesu anamwomba Baba yake wa mbinguni kuwalinda na wala si kuwaondoa duniani. Anawatuma wafuasi wake ili waweze kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha na ukweli duniani: wao ni chumvi na mwanga wa dunia. Hii ndiyo njia inayooneshwa na Mashahidi.

Baba Mtakatifu anasema, muda mfupi tu baada ya mbegu ya imani kuwa imepandikizwa nchini Korea, Mashahidi na Jumuiya ya Kikristo, walikabiliana na changamoto ya kufanya maamuzi magumu, yaani kumpokea Yesu au kukumbatia malimwengu, lakini wakaonesha ujasiri wa kuachia fahari zote ambazo zingewasababishia kuwa mbali na Yesu yaani: mali na malimwengu, fahari na heshima kwani walitambua kwamba Yesu ndiye aliyekuwa hazina yao ya kweli.

Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii bado imani inawekwa majaribuni na watu wanakabiliwa na mashinikizo makubwa ya kiimani kiasi cha kuwataka kuvuruga imani yao na mahitaji msingi ya Kiinjili, ili kuendana na walimwengu.

Mashahidi wa Korea wanalo jambo kubwa la kuwafundisha watu wa nyakati hizi kwamba, licha ya utajiri mkubwa uliopo, lakini umaskini wa hali na kipato unaendelea kukua na kuongezeka kimya kimya; kwa nadra sana kilio cha maskini kinaweza kusikilizwa; mahali ambapo Kristo anaendelea kuita anawataka wafuasi wake kumpenda na kumhudumia kwa kuwashughulikia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu mapema asubuhi siku ya Jumamosi, tarehe 16 Agosti 2014 ametembelea Madhabahu ya Mashahidi wa Seo So-Mun na kuweka shada la maua, baadaye amesali katika hali ya ukimya kwa kitambo kidogo na hatimaye, kuendelea na safari yake kwa ajili ya kumtangaza Paulo Yun Ji-Chung na wenzake kuwa Wenyeheri.







All the contents on this site are copyrighted ©.