Hakuna njia ya mkato katika maisha ya kitawa! Kuna haja ya kujisadaka bila ya kujibakiza!
Mara baada ya chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko
na msafara wake, Jumamosi, tarehe 16 Agosti 2014, Baba Mtakatifu alitembelea Kituo
cha Afya cha "House of Hope", kilichoko Kkottongnae kinachoendeshwa na Jimbo Katoliki
Cheongju.
Askofu Gabriel Bong-hun amemwelezea Baba Mtakatifu tangu kuanzishwa
kwa Jimbo hili kunako mwaka 1962, Kanisa limejielekeza zaidi katika kuwahudumia maskini,
wagonjwa na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kituo kinatoa huduma ya elimu
kwa watoto walemavu; kuna shule maalum ya watoto wenye ulemavu wa macho, viziwi na
walemavu wa viungo. Kunako mwaka 2001 Watawa kwa kusoma alama za nyakati, walianzisha
shule kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na wale waliotelekezwa
na wazazi wao kutokana na ulemavu.
Mara baada ya kutembelea kituo hiki, Baba
Mtakatifu na msafara wake walielekea kwenye kituo cha "School of Love" ili kukutana
na Watawa wanaotekeleza utume wao nchini Korea. Baba Mtakatifu katika hotuba yake
amekazia kwa namna ya pekee kabisa karama za mashirika ya kitawa na kazi za kitume,
utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini Korea. Huu ni utambulisho kwamba,
kweli wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, Mungu ndiye kiini cha wito wao, changamoto
ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wengine katika mchakato wa ujenzi wa
Ufalme wa Mungu.
Baba Mtakatifu anawataka watawa kuonesha ushuhuda wa huduma
inayojikita katika furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao ya kitawa,
ili kuwavuta wengine kumfuasa Kristo. Furaha hii inarutubishwa kwa njia ya maisha
ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na maisha
ya Kijumuiya.
Haya ni maisha yanayofumbatwa katika kazi na tafakari, mambo
yanayowasukuma watawa kuwa kweli wataalam waliobobea katika kuwashirikisha wengine
huruma ya Mungu kwa njia ya maisha ya kijumuiya. Huu ni mtindo wa maisha ambao unasimikwa
katika mashauri ya kiinjili yaani: usafi kamili, ufukara na utii, kielelezo cha furaha
ya upendo wa Mungu unaojikita katika mwamba wa huruma. Baba Mtakatifu anawahakikishia
watawa kwamba, hapa hakuna njia ya mkato, wanapaswa kweli kujisadaka kwa Mungu bila
ya kujibakiza wala kujitafuta wenyewe. Ni mwaliko wa kutoka katika undani wao.
Baba
Mtakatifu anawataka watawa kuhakikisha kwamba, wanaonesha ushuhuda wa maisha ya nadhiri
ya ufukara katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, katika ngazi ya mtu binafsi
na jumuiya katika ujumla wake. Ni wajibu wao msingi kuepuka mambo yote yanayoweza
kuwayumbisha na hivyo kusababisha kashfa kwa wengine.
Nadhiri ya ufukara katika
maisha ya kitawa anasema Baba Mtakatifu ni ukuta unaolinda maisha ya kitawa na mama
anayewasaidia kukua na kutembea katika njia sahihi ya maisha. Watawa hawana budi kuachana
na unafiki kuhusiana na nadhiri ya ufukara kwa kuishi maisha ya anasa, jambo linaloharibu
Kanisa.
Ni hatari kwa watawa kumezwa na malimwengu, kiasi kwamba huduma wanayoitoa
inakuwa kama ile inayotolewa na wafanyakazi wa mshahara kwa kujiamini na kuweka matumaini
katika uwezo wao. Mwelekeo wa namna hii unaharibu kabisa ushuhuda wa nadhiri ya ufukara
kama ilivyomilishwa katika maisha na kufundishwa na Yesu mwenyewe.
Viongozi
wakuu wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume nchini Korea, wamemkaribisha
Baba Mtakatifu Francisko na kumshirikisha changamoto wanazokutana nazo katika maisha
na utume wao katika ulimwengu mamboleo. Ili watawa waweze kuchuchumilia mafao ya wengi
na mafao ya Kanisa, kuna haja ya kutumia karama za mashirika yao pamoja na mapaji
ya Roho Mtakatifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya kijumuiya yanayojikita
katika hali ya mtu kuwa na kiasi pamoja na kuwashirikisha wengine.
Changamoto
kubwa inayowakabili watawa kwa sasa ni kupoteza utambulisho na karama zao, kwa kumezwa
na malimwengu badala ya kusoma alama za nyakati kwa njia ya upyaisho wa maisha ya
kitawa. Watawa wanaungama yote haya kwa Baba Mtakatifu kwani wanatamani kuwa kweli
ni alama ya matumaini kwa njia ya upyaisho wa maisha kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi
na jumuiya zao za kitawa.
Kanisa Katoliki nchini Korea limerutubishwa kwa njia
ya damu na tasaufi ya mashahidi, lakini hata hivyo Jumuiya ya Korea inaendelea pia
kuteseka kutokana na athari za utandawazi unaojikita katika ubepari na nguvu ya kisiasa.
Kutokana na hali kama hii, Kanisa pia linachangamotishwa kujipyaisha, kwa kuonesha
mshikamano wa dhati na watu wanaoteseka, kwa kutambua kwamba, Kanisa linatoa kipaumbele
cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.