2014-08-15 15:33:58

Waonjesheni watu wa Mungu faraja, huruma na msamaha wa dhambi!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kukutana na kuzungumza na vijana wanaoshiriki katika Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia, Ijumaa tarehe 15 Agosti 2014, wakati akirejea mjini Seoul kutoka Jimboni Daejeon, amepitia kwenye Chuo Kikuu cha Wayesuit cha Sogang, kilichoanzishwa kunako mwaka 1960 na baada ya miaka kumi hivi, kikapandishwa hadhi na kuwa ni Chuo kikuu.

Hiki ni chuo ambacho kinatoa elimu yake kwa kuzingatia misingi na mafundisho ya Kanisa Katoliki na kinapata mwelekeo wake wa kifalsafa kutokana na mafundisho ya Falsafa ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Muasisi wa Shirika la Wayesuit duniani. Ikumbukwe kwamba, hii ni safari ambayo hakupangwa kwenye ratiba ya Baba Mtakatifu, lakini ameona kwamba, inafaa.

Baba Mtakatifu akizungumza na Wayesuit wanaoishi na kufanya kazi katika Chuo hiki kikuu, kwa ufupi amewataka kuihudumia na kuifariji Familia ya Mungu nchini Korea pasi na kuitelekeza. Amewakumbusha kwamba, hii ni Familia ambayo ina majeraha makubwa yanayohitaji faraja na uponyaji wa ndani. Amesema, wakati mwingine majeraha haya ni yale yanaosababishwa na viongozi wa Kanisa wenyewe.

Baba Mtakatifu anatambua kwamba, si rahisi kuweza kutoa faraja, lakini kwa mtu anayepokea faraja hii anapata nafuu katika maisha yake. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya faraja, anamwonjesha mwanadamu matumaini na kumsamehe dhambi zake. Kwa Makleri, Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, wao ni wachungaji na kamwe si watumishi wa Serikali na kwamba, wanapaswa kuwaonjesha Watu wa Mungu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka

Na Ijumaa asubuhi, Baba Mtakatifu badala ya kutumia Helkopta kwenda kwenye maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho Jimboni Daejeon, Baba Mtakatifu ametumia Treni ya abiria iendayo kasi na hivyo kumpatia nafasi ya kukutana na kusalimiana na abiria wengine.







All the contents on this site are copyrighted ©.