“Uchungu wa mwana aujuaye ni Mzazi.” Mama mzazi yuko tayari kujitosa ili kumwokoa
na kumlinda mwanae mbele ya kila aina ya hatari. Leo tutamwona mama mmoja anayemwingiza
Yesu darasani na kumwelewesha jinsi mama anavyoujua uchungu wa kuzaa.
Kituko
kizima kilitokea Kanaani, katika nchi ya kipagani ya Tiro na Sidoni ambako Yesu alikutana
na huyo mama Mkananayo. Ili kuweza kuupata vizuri ujumbe wa kituko hicho, yabidi tujue
kilichomtoa Yesu nchini kwake Uyahudini na kumpeleka nchi hiyo ya watu wa kuja (Wapagani).
Ni
kwamba, kabla ya kutoka nchini kwake hali ya hewa haikuwa nzuri kati yake Yesu na
mafarisayo na waandishi. Yesu alirushiwa maneno ya kashfa, kwamba hakuwa anawalea
vizuri wanafunzi wake jinsi ya kufuata mapokeo ya jadi ya nchi, mathalani juu ya usafi.
Yesu naye akawarushia madonge na kuwaambia: “Ninyi ni wanafiki, kwa vile mnajizingizia
kufuata mapokeo ambayo mmejitungia wenyewe na kuacha kufuata Neno la Mungu.”
Akawatolea
mfano: “Mnajua kuna amri inayosema kwamba yatakiwa kuwatunza wazazi lakini ninyi mwasema,
kile kilichotolewa sadaka kwa Mungu ni korbani yaani ni sadaka takatifu, mapato yake
hamfanyi chochote.” Baada ya majadiliano hayo, Yesu anawaacha na anarudi nyumbani
kwake. Anapofika huko wanafunzi wake wanamtonya: “Unajua mzee, kwamba wafarisayo wamekwazika
na kile ulichowazungumzia.” Sasa, kwa vile Yesu alisha chafuka, yaani alishachukizwa
na fikra finyu za watu wake, ambazo hata mwenyewe alijisikia amebanwa nazo na zinamkosesha
hewa, akaanza kuwapasha wanafunzi wake na kuwaambia hawana akili, akitumia neno kichwa
(asunetoi): “Nanyi mnaonekana hamna kitu kabisa kichwani.”
Akaendelea kuwaambia
wanafunzi wake: “Ninyi hamwoni kuwa kila kinachomwingia mtu ndiyo kichafu kuliko kile
kinachomtoka?” Kutoka hapo anaorodhesha namna saba inayoweza kumfanya mtu awe mchafu
moyoni: “mawazo machafu, uuaji, uzinzi, ushahidi wa uwongo, rushwa, nk” kwa hiyo kutawadha
peke yake hakutoshi kumsafisha mtu na moyo mchafu wa namna hiyo. Haya ndiyo mazingira
yaliyopelekea hadi “Yesu akatoka huko”.
Tendo hilo la “kutoka au kuondoka huko”
ni muhimu sana. Hapa umetumika msamiati ule wa kitabu cha Kutoka, kulikowahusu waisraeli
walipokuwa bado utumwani Misri. Wakatoka Misri walikokuwa wamefungwa. Walihitaji kutoka
na kwenda pahala penye panapowapa uhuru. Ni neno linaloonesha mpito wa kutoka sehemu
ya kifungo ambako mtu hawezi kujikamilisha na kujitoshelesha kama binadamu na unashindwa
kujibinafasi.
Ieleweke pia kuwa Yesu Mungu nasi amechukua mwili wa binadamu.
Alizaliwa, akalelewa na kukua katika mazingira ya fikra na mila za mama wa nchi ya
uyahudi. Hivi naye anajisikia kubanwa na fikra finyu za watu wa kabila lake. Hii ndiyo
hoja, inayomfanya Yesu aondoke huko aende kwa wapagani akaone kama nao wanafanana
na picha ile ya fikra waliyonayo watu wake.
Juu ya huyu mama tungeweza pia
kujiuliza: “Hivi huyu ni mama wa namna gani? Halafu tena ni kwa nini afike mama na
siyo baba wa mtoto kama ilivyotokea Kafarnaumu kwa yule Senturione aliyefika kumwomba
Yesu juu ya mtoto wake?” Jibu ni kwamba mama huyu anaiwakilisha nchi yoyote ile ya
kipagani isiyokutana na Kristo. Nchi ya namna hiyo ipo gizani yaani imepagawa na uovu
na vurugu za kishetani. Ni ubidamu uliopagawa na shetani anayenyanyasa na kunyima
wengine utu wao.
Mama huyu anamkaribia Yesu na kumlilia: “Unirehemu Ee Bwana
Mwana wa Daudi, mtoto wangu amepagawa na shetani.” Baada ya ombi hili tungetegemea
Yesu anainuka na kwenda mara moja nyumbani kwa mwanamke huyu na kufanya muujiza wa
kumfukuza huyo shetani. Kinyume chake, tunavishuhudia vituko ambavyo ni vya muhimu
kuvifuatilia. Kituko cha kwanza unamwona Yesu anamchunia mwanamke bila kusema neno
lolote. Kituko hiki cha Yesu kumkalia kimya mama huyu kinawakilisha fikra za watu
wa kabila lake la wayahudi.
Yaani, tabia ya kutojali shida za watu wasio wa
kabila lako na wa dini yako. Yesu anaonekana kuendeleza tabia aliyoirithi dhidi ya
wapagani. Ni kweli, mwanzoni mwa shughuli zake Yesu hakushughulika na ulimwengu kijumla
kama atakavyosema mwenyewe, kwamba, inabidi ajali zaidi wokovu wa watu wake. Baada
ya Yesu kumkalia kimya, kinafuata kituko kingine toka kwa wafuasi wake kinachodhihirisha
waziwazi tabia ya kuwatenga wapagani, kwa jinsi wanavyoongea vibaya dhidi yake: “Mfukuzie
mbali mama huyu anatupigia-pigia makelele”.
Wanafunzi hawa na mwalimu wao hawakulielewa
bado hitaji la ulimwengu wa kipagani juu ya ukombozi utokao kwa Neno la Mungu. Wanataka
kumfukuza mama huyu bila hata ya kuhojiana naye na kuelewa dukuduku iliyomo moyoni
wake. Baada ya wanafunzi kituko kinachofuata Yesu anazidi kukandamiza zaidi hoja yake
anapowaambia wanafunzi: “Mimi sijatumwa isipokuwa kwa kondoo waliopotea wa Israeli.”
Yule
mama bila kujali, akaendelea kumpigia Yesu magoti na kumsihi: “Bwana unisaidie”. Hivi
ndivyo lilivyo ombi la wapagani la kuomba kupokea Neno la Mungu. Kwa hiyo endapo Uyahudi
ni Mama (utu, ubinadamu), hata Upagani ni Mama (utu, ubinadamu) unaohitaji Neno linalofukuza
mashetani ya ulimwengu huu wa kipagani, yaani ushetani wa vita, wa uonevu, wa kutesana,
wa utumwa, nk. Hapa mwanamke huyu anaelewa fika kwamba, ili kufukuza aina hii ya ushetani
unahitaji Neno la mtu kama huyu Yesu wa Nazareti.
Baada ya king’ang’anizi
cha mama huyu, kituko kinachofuata Yesu anaamua kumtolea lugha ngumu zaidi mama huyu:
“Siyo vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Mbwa anayetajwa hapa ni
yule wa kufugwa siyo mbwa koko. Wapagani walieleweka kuwa kama mbwa wa kufugwa. Kwa
hiyo, katika nyumba moja watoto hawakutakiwa kula chakula sahani moja na mbwa wa kufugwa.
Na chakula kinachomaanishwa hapa ni Mwanga, ni Neno la wokovu hilo labidi
waangaziwe wayahudi tu. Pepo au shetani huyo mchafu anatakiwa atolewe kwa Wayahudi
tu. Kwa tamko hilo la Yesu, Mama huyu akatambua kuwa kijana huyu hajakua bado. Kwa
sababu Yesu ilimbidi akue katika umri, katika hekima na neema ya kuelewa mpango wa
Mungu wa kuukomboa ulimwengu mzima, yaani apanuke katika umisioni ambao ameitwa kuutangaza.
Kwa hiyo akiwa kama mama kweli, mwanamke huyu anasimama kidete na kuanza kumsomesha
Yesu.
Kwanza anayakubali maneno ya kumlinganisha yeye na mbwa, lakini anaongeza
kumwelewesha kwamba “Kwa mbwa vinawatosha vipande vinavyoanguka chini ya meza wanayokula
watoto.” Ujumbe huu “Yatosha vipande” ni muhimu sana. Mama huyu anaona kwa ajili ya
kuishi watoto wake vinawatosha vipande tu vya chakula anavyowagawia watoto wake (wayahudi
-waisraeli).
Jibu hilo ni sawa na alichokisema Yesu mwenyewe kwamba imani
ni kama mbegu ya haradali (ndogo sana) lakini inaweza kukua na kufanya muujiza mkubwa.
Mwanamke huyu anaelewa kwamba, ili kumponya mtoto, yaani ili kumfukuza pepo huyu anayekandamiza
ubinadamu wetu “vinatosha vipande” tu. Jibu la mama huyu linamtoa Yesu kutoka kwenye
fikra finyu za kiyahudi alizokulia nazo. Yesu anafunguka akili na angeweza tu kusema
“mama ujumbe nimeupata” badala yake anaishia tu kushangaa na kumwambia mwanamke yule:
“imani yako ni kubwa, utendewe kama unavyotaka”.
Yesu anashangaa kuona jinsi
binadamu wa ulimwengu wa kipagani walivyo na imani kuu kwa Neno lake kwamba lina uwezo
wa kufukuza aina zote za pepo. Ukuu wa imani ya mama huyu upo katika kuamini kwamba
Mungu ni kama mama aliye na uchungu na watoto wake. Mama huyu hana imani kali ya kitaalamu,
bali ana imani ya mama mwenye uchungu na watoto wake.
Anamfahamu kwa undani
Mungu kuwa yu kama mama na anaungana naye katika moyo wake wa umama. Yaani ni Mungu
anayeonja maumivu ya vidonda vya waana wake. Ama kweli “Uchungu wa mwana aujuaye mzazi”.
Na Mungu ndiye mzazi mkuu. Mungu aliye mama anafurahi anapomwona mama yeyote mwenye
furaha. Mungu ana uchungu anapomwona mama yeyote kuwa na uchungu kwa mtoto wake. Mama
huyu anasadiki kwamba haki kuu mbele ya Mungu ipo katika kuteseka na mwenye kuteseka.
Haki hiyo ni kwa ajili ya watoto wote wa Mungu, iwe watoto wa wayahudi, watoto wa
wakanaani, watoto walio ndani ya kanisa au nje ya kanisa, watoto walio bara au walio
visiwani.
“Imani yako ni kubwa” hayo ni maneno sahihi kabisa katika ulimwengu
wa leo. Imani namna hiyo haina dini wala utaifa. Kuna wamama wengi kama huyu mkananayo
ambao hawajui kusali kanisani wala kuswali msikitini, lakini wanaujua moyo wa kimama
alio nao Mungu. Wako wamama wengi leo wasiolijua jina la Mungu, bali wanajua kwamba
Mungu anao moyo wa kimama. Huyo mama Mungu ni wa sisi watoto wake wote tunaoteseka
ulimwenguni.
Kwa hiyo ujumbe tunaopata leo ni huu kwamba, ulimwengu unasubiri
Neno linalouponya kutokana na kila aina ya ushetani unaomnyima utu binadamu. Na Neno
hilo ni Yesu mwenyewe. Kinatosha kipande kidogo tu cha imani kwa Yesu ili kuweza kutenda
muujiza.Yesu anatualika sisi leo tuwe kama yeye, yaani tuwe na uchungu kwa jamii zetu
kama “mama alivyo na uchungu kwa mwana wake”. Uchungu wa kuiona njaa ya watoto (jamii)
na kuituliza.
Ujumbe mwingine ni kwamba Yesu anatoka, anatembea na kukua katika
imani, anajifungua kwa mkananayo wa Tiro na Sidoni, na hivi "anabangatuliwa" akili
na mwanamke huyu mpagani. Anatufundisha kutambua kwamba binadamu mwenye hekima ni
yule aliye kama Yesu anayetoka na kwenda kujifunza toka kwa kila mtu. Nasi tuwe na
hekima kama ya Yesu ya kuwa tayari kutoka na kwenda kujifunza toka kwa kila mtu hata
yule tunayemdhani kuwa ni mchovu.