2014-08-15 10:10:53

Kijana usiwe bendera kufuata upepo! Utakiona cha mtema kuni!


Baba Mtakatifu Francisko anaonesha matumaini makubwa kwa vijana na kumbe vijana nao wanapaswa kuhakikisha kwamba, hawamwangushi Baba Mtakatifu katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Baba Mtakatifu katika maandalizi ya maadhimisho ya Siku za Vijana Kijimbo na Kimataifa anawataka kutafakari kwa kina na mapana Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kwa wanafunzi wake. RealAudioMP3

Padre Tumaini Litereku Ngonyani kutoka Jimbo kuu la Songea, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha changamoto ambazo vijana wanakabiliana nazo katika maisha kwa kutambua kwamba, vijana wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa ndiyo maana Kanisa linaendelea kuwekeza katika majiundo makini kwa vijana, ili waweze kuwa kweli ni vyombo vya Uinjilishaji kati ya vijana wenzao.

Padre Ngonyani anasema Baba Mtakatifu Francisko anawapatia changamoto kubwa vijana ya kuhakikisha kwamba, kamwe hawamezwi na malimwengu. Wawe ni watu wenye msimamo thabiti wa imani, maadili na utu wema. Vijana wajitahidi kuridhika na kile wanachokipata kwa juhudi na maarifa, wajitahidi kuondokana na kishawishi cha uchu wa mali na tamaa ya fedha ya haraka haraka; mambo yanayozaa dhambi na kuporomoka kwa maadili na utu wema.

Padre Ngonyani anawataka vijana kuwa na kiasi, kuridhika na kile wanachokipata kwa njia za halali; kuongeza juhudi, maarifa na ujuzi katika masomo na kazi, ili kweli kile wanachokipata kiwe ni matunda na jasho lao. Vijana wajitahidi kupambana na umaskini wa hali na kipato kwa kujikita katika ufukara unaonesha hali ya kujikatalia pasi na kumezwa na malimwengu. Kwa vijana wenye msimamo wa maisha, hao machoni pa wengi ni watu waliopitwa na wakati, wajinga pengine hata wanaitwa kuwa ni maskini.

Lakini, vijana wakumbuke kwamba, mtu mwenye msimamo na imani thabiti katika maisha yake ataheshimiwa hapa duniani na kupata furaha katika maisha ya uzima wa milele. Vijana wenye maadili na utu wema ni matajiri wakubwa machoni pa Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.