Iweni chachu ya mabadiliko duniani bila kumezwa na malimwengu!
Baba Mtakatifu Francisko, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa
mbinguni mwili na roho sanjari na maadhimisho ya siku kuu ya uhuru wa Korea, Ijumaa
tarehe 15 Agosti 2014 akiwa Jimboni Daejeon, Korea ya Kusini ameadhimisha Fumbo la
Ekaristi Takatifu kwenye Uwanja wa michezo wa kimataifa.
Baba Mtakatifu amekutana
pia na kuzungumza na watu walioathirika katika ajali ya Meli iliyotokea hivi karibuni
huko Sewol na kusababisha vifo vya watu 293, kati yao 10 hawajulikani waliko hadi
sasa. Meli hii ilikuwa imebeba abiria 476.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake
amekazia dhamana na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo
cha hatima ya watoto wateule wa Mungu na viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani
Kanisa. Anatambua nafasi ya Bikira Maria kama mwombezi na Mama wa Kanisa nchini Korea.
Anamwomba ili aweze kuwakirimia ule uhuru waliojaliwa na Mama Kanisa kwa njia ya Sakramenti
ya Ubatizo, ili aongoze juhudi zao katika mchakato wa kuleta mabadiliko duniani mintarafu
mpango wa Mungu pamoja na kuliwezesha Kanisa kuwa ni chachu ya Ufalme wa Mungu nchini
Korea.
Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Bikira Maria awawezeshe Wakristo
nchini Korea kuwa kweli ni nguvu ya kuleta mabadiliko ya maisha ya kiroho katika medani
mbali mbali. Wakristo wapambane dhidi ya malimwengu yanayotaka kumeza tunu msingi
za maisha ya kiroho na kitamaduni, kwa kuchochea mashindano yasiyokuwa na tija wala
mashiko ambayo hatima yake ni ubinafsi na kinzani.
Watu wawe na ujasiri wa
kukataa mifumo ya elimu ambayo inasigana na utu wa binadamu, kiasi cha kusababisha
umaskini, utengano wa wafanyakazi pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo usiothamini
ile sura na mfano wa Mungu, chemchemi ya maisha; mambo yanayodhalilisha utu na heshima
ya binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anawaambia Wakatoliki nchini Korea kutambua
kwamba, wameitwa na wanapaswa kuthamini urithi wao, ili kuwa tayari kuwarithisha vijana
wa kizazi kipya. Hii ni dhamana inayojikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kuambatana
na Neno la Mungu, kwa kushikamana na maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa
Jamii.
Matumaini yanayobubujika kutoka katika Injili ni dawa tosha kabisa
dhidi ya hali ya kukata tamaa, inayoendelea kujitokeza miongoni mwa watu kama Saratani.
Jamii kwa nje inaonekana kuwa ni tajiri, lakini ndani yake inajikuta kwamba, ina ukakasi
na utupu wa maisha. Hali ya kukata tamaa imewaathiri vijana wengi.
Mara baada
ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala
ya Malaika wa Bwana amewakabidhi wananchi wa Korea chini ya ulinzi na usimamizi wa
Bikira Maria, hasa wale waliopoteza ndugu na jamaa zao kwenye ajali ya Meli iliyotokea
Sewol. Ajali hii ilikuwa ni alama ya mshikamano wa kitaifa katika majonzi, changamoto
ya kuendelea kushirikiana kwa pamoja, kwa ajili ya mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu
anawaweka chini ya ulinzi, usimamizi na maombezi ya Bikira Maria watu wote wanaoteseka
hasa wagonjwa, maskini na watu wasiokuwa na fursa za ajira. Anamwomba Bikira Maria
kuwafariji wale wote ambao bado wanaendelea kubeba makovu ya ukosefu wa haki wakati
wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Baba Mtakatifu mwishoni, anawaweka vijana wote kutoka
Barani Asia, wanaoadhimisha Siku ya sita ya Vijana Barani Asia chini ya ulinzi wa
Bikira Maria. Anawataka wawe ni mwanga angavu wa dunia inayokumbatia amani kadiri
ya baraka ya Mwenyezi Mungu.
Wakati huo huo, Askofu Lazzaro You Heung-sik
wa Jimbo Katoliki la Daejeon katika hotuba yake ya shukrani amekumbushia hija za kitume
zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili nchini Korea na mabadiliko yaliyojitokeza
katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi chote hiki. Kanisa Katoliki nchini
Korea limejielekeza zaidi na zaidi kuwa ni Kanisa linaloshirikishana na wengine utajiri
na rasilimali zake. Bado Korea inaogelea katika kinzani za kijamii na kisiasa, bado
inawaombolezea watoto wake walizama na kufariki dunia baharini.
Katika mazingira
magumu na tete kama yaliyoko kwa sasa nchini Korea, waamini wanafarijika kwa Neno
la Mungu linalowachangamotisha kwa kuwaambia, ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako
imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia. Waamini wa Korea wanawaomba Mashahidi wa
imani kutoka Korea waliopokea zawadi ya imani, wakaishi kwa upendo bila kuogopa kujisadaka
katika maisha, wakawa tayari kumfuasa Mwalimu na Bwana wao Yesu Kristo, kwa kushuhudia
imani katika matendo, wawe ni waombezi wao wa daima.
Askofu Lazzaro mwishoni
anasema kwamba, kwa hakika waamini na watu wote wenye mapenzi mema wameadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu, wamesali Rozari Takatifu na kwa pamoja wamesali sala maalum kwa
ajili ya maandalizi ya ujio wa Baba Mtakatifu nchini Korea.