Askofu Lazzaro You Heung-sik wa Jimbo Katoliki la Daejeon, Mwenyeji wa maadhimisho
ya Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia, akimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwenye
Madhabahu ya Solmoe anasema, ni furaha kuu isiyokuwa na kifani kuwakaribisha wageni
waliofika kutoka mbali, lakini kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko.
Madhabahu
ya Solmoe ni mahali alipozaliwa Mtakatifu Andrea Kim Daegeon, Padre wa kwanza wa Kanisa
Katoliki nchini Korea, aliyezaliwa na kukumbatia imani bila ya uwepo wa Wamissionari,
mfano wa pekee kabisa duniani! Hapa ni mahali ambapo mashahidi wengi wa imani wameteswa
na kuuwawa kikatili, ni watu walioonesha ushuhuda wa imani katika matendo.
Kongamano
la Sita la Vijana Barani Asia ni changamoto ya kichungaji kwa Wakristo na Wakatoliki
kwa namna ya pekee kabisa kwani Kanisa linakabiliwa na changamoto mbali mbali katika
maisha na utume wake. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ni mambo yanayopelekea
kumong'onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kimaadili na utu wema na mateokeo yake
ni watu kukumbatia utamaduni wa kifo na uharibifu wa mazingira.
Hii ndiyo
changamoto kwa Wakristo kuwa kweli ni mashahidi kwa kuchagua na kukumbatia ukweli
unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha, ili kushinda vishawishi vinavyowazunguka.
Wakristo kwa kufuata mfano wa mashahidi na mwanga wa Injili wanapaswa kuwasha mwanga
wa imani kwa kufanya maamuzi ya maisha na kuyatolea ushuhuda kwa kujikita katika imani
thabiti kama walivyofanya Mashahidi wa Korea waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na
Kanisa lake, huku wakipambana na ukanimungu, utamaduni wa kifo, uchu wa mali na madaraka.
Askofu
Lazzaro You Heung-sik anahitimisha hotuba yake ya makaribisho kwa Baba Mtakatifu kwa
kumwomba asonge mbele ili kuinjilisha Ulimwengu na Kanisa, wao wako nyuma yake na
wana muunga mkono.
Baba Mtakatifu kwa umakini mkubwa amesikiliza shuhuda ambazo
zimetolewa na vijana Cambodia, Hong Kong na Korea waliomshirikisha kuhusu ndoto za
maisha yao wakitaka kuwa Mapadre ili kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwatangazia
watu Injili ya Furaha, lakini bado hawana msingi thabiti wa imani. Vijana wanakabiliana
na changamoto nyingi za kiimani, kimaadili na utu wema. Kuna baadhi ya nchi hazina
uhuru wa kidini, Je, kama vijana wajibu na utume wao ni nini?
Kanisa lina
watakatifu lakini pia limejaa wadhambi, zote hizi ni changamoto za maisha, ili kutubu
na kuongoka, ili kuonja huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Vijana wengi wanaonekana
kana kwamba, wamechanganyikiwa kutokana na kumezwa mno na malimwengu, kinzani pamoja
na kujisikia kuwa ni wanyonge. Yote haya yanapelekea kuongezeka kwa uhalifu na vijana
kujinyonga; kwa ufupi vijana wengi wamechanganyikiwa kiasi cha kukosa utambuzi wa
tunu msingi katika maisha chemchemi ya furaha ya kweli. Korea bado imegawanyika, watu
wanaishi katika chuki na uhasama. Hizi ni baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo
vijana Barani Asia.