2014-08-14 15:24:01

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 20 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa mteule wa Mungu, karibuni tutafakari pamoja Neno la Mungu Dominika ya 20 ya mwaka A wa Kanisa. Wewe nami leo, tunaalikwa kutambua kuwa wokovu ni kwa ajili ya wote, ndiyo kusema tunahabarishwa habari njema yakuwa Kanisa lililo Katoliki ni kwa ajili ya watu wote, liko milango wazi, ni chombo cha wokovu kwa ajili wanadamu, viumbe wateule wa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo kila mmoja wetu anadaiwa imani na kudumu katika kuomba na kusali kama mama yule mkananayo tunayemsikia katika injili. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza toka kitabu cha nabii Isaya, tunaona jinsi Wana wa Israeli baada ya kukaa utumwani Babilonia wanaanza kugundua kuwa wapagani si mashetani kwa asili, bali nao wanayo maisha ya adili, shida ni kwamba hawajaamini katika Mungu mmoja wa Waisraeli. Dini ya wapagani haikuwa ubatili wala uozo bali ilikuwa na sheria kadhaa zilizokuwa zinaonesha uadilifu na namna ya kuhusiana kijamii. Jambo hili limewasaidia Waisraeli kubadili mtizamo wao wa kiutu na kidini uliokuwa hauruhusu mtu mwingine asiye mwisraeli kuingia na kushiriki mfumo wao wa kidini na namna yao ya kufikiri!

Nabii Isaya anaishi katika kipindi cha utumwa wa Babilonia, yupo pamoja na Waisraeli wenzake na hivi anajifunza kufungua moyo wake kwa umoja wa wanadamu wote. Tokana na hili anawafundisha wana wa Israeli kuwa hakuna haja tena ya kuweka mipaka katika suala la imani bali kushirikiana pamoja ili kumtukuza Mungu mmoja. Anawaalika wote kutambua kuwa jambo la msingi ni kushika sheria ya Bwana na kutenda haki na kwa njia hii, wokovu wa Bwana u karibu na awaye yote awe myahudi au mtu wa mataifa.

Wale watakaoshika sheria ya Bwana watatukuka na kungaa katika mlima wa Bwana na wataingia katika nyumba ya sala iliyo nyumba ya Mungu. Hakuna awaye yote ashikaye sheria ya Bwana atakayekuwa mgeni katika safari ya wokovu.

Jambo la umoja katika kushiriki habari ya wokovu linakaziwa zaidi katika somo la Injili pale ambapo tunamwona Bwana akiongea na mwanamke mkananayo. Mama huyu si myahudi, na hivi yuko katika upande wa mataifa au wapagani. Akiwa amejaa imani na matumaini kwamba Bwana ana nguvu na hivi atamponya bintie, anasali sala akipaza sauti akisema “unirehemu Bwana Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana ana pepo”.

Ni sala ya kuomba huruma na msamaha toka kwa Bwana, na kweli mama huyu anapata jibu la ombi lake. Kabla ya kutimiziwa shida yake yapo mambo ya kukagua na hasa imani kama ni sahihi! Kwanza Bwana anaonekana kutomjali na anamwambia maneno ya kumkatisha tamaa, “Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kumtupia mbwa”. Hata hivyo mama huyu anazidi kuomba akisema hata mbwa hupokea makombo yanayodondoka chini ya meza za mabwana wao! Hili laonesha kuwa hata wasiowaisraeli waweza kupokea imani na wokovu wa Mungu. Bwana akipendezwa na imani ya mama huyu mkananayo anamwambia utimiziwe shida yako na binti yake akapona.

Kwa nini Bwana anatumia njia ndefu namna hii katika kuleta habari njema kwetu? Kwa hakika anataka Mitume na watu wengine waelewe vema mabadiliko thabiti toka fikira potofu za kiyahudi zinazosistizia ukabila na waelekee katika umoja kamili wa wana wa Mungu. Anawaambia wayahudi kuwa anataka wokovu kwa ajili ya wote. Anaonesha dosari ambayo Mitume wanapaswa kupambana nayo katika utume wao.

Ni katika mantiki hiyo Mtume Paulo anatufundisha kuwa kwa Waisraeli kukataa Mwana wa Mungu ilikuwa ni kosa ambalo lilifungua mlango wa wokovu mapema zaidi kwa mataifa mengine. Ingekuwa pengine vigumu Neno la Mungu kuenea haraka ulimwenguni kote kama Wayahudi wangelikubali haraka hasa tukitambua hali yao, yaani ugumu katika kuwapokea wengine wasio wayahudi. Zaidi ya hilo kuna wayahudi wamepokea imani kwasababu ya wongofu wa mataifa.

Ndugu yangu mpendwa ninakualika kutambua kuwa wokovu si kwa ajili ya mtu mmoja bali kwa ajili ya wote. Hili latueleza vema kuwa kazi ya kimisionari ya Kristu kwa njia ya Kanisa lake ni kwa ajili ya mataifa yote. Ndiyo maana Mababa Watakatifu wa zama zetu wanakazia utume wao wa kimisionari kwa njia ya mafundisho halisia ya kwenda katika mataifa kama mtume Paulo. Wanaitika vema Neno la Kristu alilomwambia Mt Petro “ukawaimarishe ndugu zako” Nasi vivyohivyo tukazie mbiu hiyo katika utume wetu katika ulimwengu wa leo. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.