Shirika limekuwa na kuchanua, matunda yanaanza kuonekana!
Miaka ishirini na mitano ya Shirika la Masista wa Pendo la Huruma wa Mtakatifu Vinsenti
wa Paulo, Mitundu - Singida ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya
ustawi na ukuaji wa Kanisa nchini Tanzania, hususan eneo la Mitundu ambalo kwa wengi
lilidhaniwa kuwa ni pembezoni mwa jamii, lakini huko ndiko ambako Shirika limejikita
na sasa matunda yake yanaanza kuonekana kwa kusherehekea Jubilee ya Miaka 25 ya uwepo
wao nchini Tanzania.
Tunaposherehekea tukio kubwa la kihistoria katika Shirika
letu, yaani Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa Shirika hapa Mitundu – Tanzania,
kama familia ya kivinsenti tunaalikwa kumwinulia Mungu Mtakatifu mioyo yetu na kusema
asante kwa makuu aliyotutendea.
Ufalme wa Mungu umefanana na punje ya haradali
nayo ni ndogo kuliko mbegu zote lakini ikiisha kumea huwa kubwa kuliko mimea yote
hata ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake (Mt.13:31-32).
Hivyo
tunapotafakari matendo makuu aliyotutendea Mungu tumeona ni vema tutafakari na kutembea
katika Maandiko haya Matakatifu, tukiyafananisha na ukuaji wa Shirika letu hatua kwa
hatua ndani ya Maongozi ya Mungu.
„Maongozi ya Mungu yametuleta hapa“ (maneno
ya Mtakatifu Vinsenti wa Paulo).Waasisi wetu waliisikia sauti ya Mungu na katika fumbo
Mungu alifunua mpango wake kwa:
kusia mbegu ndogo mithili ya mbegu
ya haradali katika kitalu kidogo. Huyu ni Sr. Maria Kitiku. Yeye amekuwa mwanzo wetu
na asili yetu. Tunajivunia ujasiri na uthabiti wake, uwezo wa Mungu daima ulikuwa
ndani ya mwanzo huo. Mche huo ulianza kukua na kustawi vizuri (ongezeko la Shirika). Kuna
nyakati ambazo mche huu ulisongwa, jua kali, upepo na mvua kubwa, dhoruba na mawimbi
makali baadhi ya miche ilikosa nguvu ya kuendelea mbele. Watunza bustani wakakumbuka
maneno ya Mt. Vinsenti wa Paulo yasemayo „kama yote yanakwenda kadiri tunavyotaka
sisi, hiyo ni alama ya kukataliwa“. Katika haya yote imani, uvumilivu na utii wa Maongozi
ya Mungu yalikuwa dira yao.
Katika hayo yote Mungu alitaka kuonesha ukuu
wake na uwezo wake: „Kwa subira yenu mtayaokoa maisha yenu “(Mk 13:13). Na Mtakatifu
Vinsenti wa Paulo anasema: „Uvumilivu kidogo na tazama yamepita“.
Mungu kwa
wema na upendo wake akayahuisha matumaini ya mche kwa kuupa ustawi tena. Hapa tunayatafakari
maneno ya hekima ya Mt. Vinsenti yasemayo: „Tunahitaji neema kwa kuanza lakini zaidi
kwa kudumu“
Mmea huu sasa ni mkubwa unavutia wengi na kuwapa
watu wa ndani na nje; wa karibu na wa mbali, faraja, tumaini, furaha na kuburudisha
nafsi na mioyo ya watu. Kivuli chake chaleta amani na utulivu kwao wakaao chini yake.
Hakika tunaweza kushuhudia kwamba uwepo wa Mungu umekuwa pamoja nasi.
Mungu
upokee sifa na shukrani kwa baraka na neema zako maridhawa ulizoutendea mtii huu ambao
unazaa matunda yanayogawanywa kwa maskini. Katika Mwaka huu wa Jubilei tutembee
hatua kwa hatua tukialikwa kuyapokea maisha ya wito, kuyaendeleza na kuyapa sura stahiki.Tunatumwa
katika yote kumpa Mungu kipaumbele na Injili ya Mwanaye na kuwafanya wanadamu na hasa
maskini wakutane na Pendo la Huruma. Mungu libariki Shirika letu. Mungu wabariki
waasisi wetu. Mungu tubariki sisi sote.