2014-08-14 11:21:44

Maaskofu wanachangamotishwa kuwa ni walinzi wa kumbu kumbu na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Korea amekazia kuhusu mambo makuu mawili yaani kama Maaskofu wamepewa dhamana ya kulinda kundi la Kristo katika kumbu kumbu na matumaini, kwa kutambua kwamba, wao ni kizazi na urithi wa kishujaa ulioneshwa katika imani kwa Kristo, utume ambao umefanywa kwa umakini mkubwa na waamini walei.

Kanisa nchini Korea ni matunda ya watu kukutana moja kwa moja na Neno la Mungu, ambalo limemwilishwa katika maisha na vipaumbele vya waamini. Ni Neno ambalo limechochea wongofu wa ndani na upyaisho wa maisha unaojikita katika mapendo, kama ilivyooneshwa na wazee wa kizazi kilichotangulia.

Haya ni matunda ya uhai wa Kanisa unaojionesha katika Parokia, Vyama vya kitume, malezi kwa vijana wa kizazi kipya shuleni, seminarini na katika vyuo vikuu ambamo Katekesi makini inakaziwa kwa namna ya pekee. Kanisa nchini Korea linaheshimiwa sana kutokana na utume wake katika maisha ya watu kiroho, kitamaduni pamoja na mwamko na ari ya kimissionari.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa ni walinzi wa hazina kubwa ya neema waliyoipokea; kutumia rasilimali ya maisha ya kiroho ili kukabiliana kwa mwono mpana na matumaini makubwa ahadi na changamoto zijazo. Maisha na utume wa Kanisa nchini Korea unapimwa mintarafu Mwanga wa Injili na mwaliko wa kumwongokea Yesu Kristo kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayewezesha ukuaji makini wa mwamini.

Haya ni matunda ya uvumilivu na udumifu katika kazi kama ilivyojionesha siku za nyuma na kama ilivyo kwa sasa. Kumbu kumbu endelevu ya mashahidi wa imani haina budi kuonesha ukweli na wala si kielelezo cha ushindi. Waamini waangalie historia yao na wawe tayari kumsikiliza Mwenyezi Mungu, ili kujikita katika hija ya maendeleo ya maisha ya kiroho.

Maaskofu wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa ni walinzi wa matumaini yanayobubujika kutoka katika Injili na neema pamoja na huruma ya Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Hii ni changamoto kwa waamini kuwatangazia walimwengu hazina kubwa na ya kweli inayompatia mwanadamu ukamilifu wa maisha. Matumaini haya yanaweza kulindwa kwa kuendelea kuwasha moto wa utakatifu wa maisha, upendo wa kidugu, ari ya kimissionari na umoja wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu Katoliki nchini Korea kujenga Kanisa la Kimissionari ambalo liko tayari kutoka kwenye pembezoni mwa jamii mamboleo ili kujenga vionjo vya maisha ya kiroho, vinavyowawezesha waamini kujitambulisha kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kipaumbele cha pekee, kitolewe kwa watoto pamoja na kuzima kiu ya matamanio ya vijana, kwa kuwaenzi wazee ambao ni hazina ya hekima na mang'amuzi.

Kama walinzi wa matumaini wanapaswa kuonesha ushuhuda wa kinabii kwa kujenga mshikamano wa upendo na udugu kwa wakimbizi, wahamiaji na wote wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa lijikite katika mchakato wa maendeleo endelevu katika jamii, ili kutengeneza fursa za ajira na nafasi za elimu. Huduma za kijamii zinazotolewa na Mama Kanisa ziwasaidie watu kukua na kukomaa kama binadamu, ili kumwezesha mtu kuonesha utu wake, ugunduzi na utamaduni.

Hapa kuna haja ya kukuza na kujenga dhana ya Kanisa maskini kwa ajili ya maskini, kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, dhana hii ya Kanisa la Mwanzo itaendelea kuliunda Kanisa la Korea kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, ushuhuda wa Kiinjili unachangamoto zake hususan kwa Kanisa nchini Korea, mahali ambapo Kanisa linaishi na kutekeleza utume wake miongoni mwa watu wenye uwezo lakini wako kwenye hatari ya kumezwa mno na malimwengu.

Kutokana na mwelekeo kama huu, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa makini kwa kuchagua mtindo wa kuratibu, kupanga na kutumia mali ya dunia hii. Ni watu wanaopaswa kuwa pia na mtindo wa maisha unaowawezesha kutomezwa na malimwengu, uchu wa mali na madaraka, bali kwa kujikita katika kanuni msingi za Injili ya Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.