2014-08-14 10:07:06

Lengo la hija ya kitume ni: kushiriki maadhimisho ya Siku ya VI ya Vijana Barani Asia na Kuwatangaza Watumishi wa Mungu 124 kuwa Wenyeheri!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuzungumza na viongozi wa serikali nchini Korea na Mabalozi wanaowakilisha nchini zao, amemtembelea Rais wa Korea ya Kusini Bibi Park Geunhye katika Ikulu yake inayojulikana kama "Blue House". Nyimbo za nchi hizi mbili zimepigwa na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akakagua gwaride la heshima na baadaye viongozi hawa wawili wamefanya mazngumzo ya faragha pamoja na kubadilishana zawadi.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali ya Korea ya Kusini amegusia malengo makuu mawili, yaani kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya VI ya Vijana Barani Asia, hii ni sherehe ya imani inayowaunganisha vijana wakatoliki kutoka nchi mbali mbali Barani Asia. Lengo la pili ni kuwatangaza Watumishi wa Mungu 124 kutoka Korea kuwa ni Wenyeheri. Hawa si wengine bali ni Paul Yun Jichung na wenzake 123.

Baba Mtakatifu anawapongeza wananchi wa Korea kwa kuwathamini wazee kwa kuwaenzi na kuwashirikisha katika maisha ya kijamii. Ni jamii inayopenda na kuheshimu mapokeo yake pamoja na kuwathamini vijana, ili kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kijamii ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za nyakati hizi. Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee wananchi wa Korea kutafakari kwa makini namna bora zaidi ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kijamii, ili kuunda jamii wanayokusudia.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake anagusia pia: amani, upatanisho na utulivu nchini Korea na kwamba, hii ni changamoto kubwa na endelevu kwa wanadiplomasia kuhakikisha kwamba, wanavunja kuta za utengano na chuki, ili kujenga utamaduni wa upatanisho na mshikamano wa dhati; mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.

Amani anasema Baba Mtakatifu, si ukosefu wa vita na kinzani bali ni kazi ya haki inayojikita katika msingi wa kuheshimiana, kuelewana na upatanisho. Uzoefu katika ulimwengu wa utandawazi unawataka watu kufahamiana, ili kutafuta mafao ya wengi na maendeleo ambayo yanapaswa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiuchumi na kiutu.

Baba Mtakatifu anasema katika mchakato wa maendeleo, nchi zilizoendelea duniani zinakabiliana na matatizo na changamoto nyingi za kijamii, migawanyiko ya kisiasa, ukosefu wa usawa kiuchumi pamoja na kuwa na matumizi sahihi na yanayowajibisha kutunza mazingira.

Baba Mtakatifu anawahimiza viongozi nchini Korea kujitahidi kujenga utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa watu wasiokuwa na sauti pamoja na kuwasaidia kupata mahitaji yao msingi, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukuaji wao kiroho na kiutu.

Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena anakazia utamaduni wa utandawazi unaojikita katika mshikamano, ukiwa na lengo la kukoleza maendeleo ya kila mwanafamilia ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, ni hamu ya Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Korea kushiriki kikamilifu katika maisha ya taifa lao.

Kanisa linapenda kuchangia katika sekta ya elimu kwa vijana, ukuaji wa ari na moyo wa mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuwa ni raia wema kwa kuwarithisha hekima na busara kutoka kwa mababu zao na katika imani, ili kukabiliana na changamoto za kisiasa na kijamii zinazojitokeza nchini mwao.







All the contents on this site are copyrighted ©.