2014-08-14 13:02:03

Korea yahitaji baraka za Papa kujenga amani na maridhiano-Maaskofu


Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya kukutana na uongozi wa kisiasa katika Makazi ya Rais wa Korea Kusini, ameikamilisha ratiba ya hadhara ya siku ya Alhamisi kwa kukutana na Maaskofu wote wa Korea. Ujumbe wa kumkaribisha Papa, umetolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea , Askofu Peter Kang U-il wa Jimbo la Katoliki la Cheju .

Katika hotuba hiyo, Askofu Kang, amemshukuru Papa kwa moyo wake wa majitolea yenye upendo mkuu katika huduma za Kanisa, huku akionyesha kutambua kwamba, ameitembelea rasi ya Korea licha ya kuwa kipindi cha joto kali. Na kwamba wanafahamu vyema kwamba, hata amejinyima likizo yake binafsi. Na hivyo wote wanawiwa kutoa shukrani zao za dhati, kwa moyo wake wa kibaba na upendo wake kidugu usio na kipimo.

Askofu Kang aliendelea kumwambia Papa kwamba, Wakorea wote wamekuwa wakisubiri kwa ujio huu wa Papa , si tu kwa Wakatoliki Wakorea, lakini Pia watu wote Korea, wamekuwa na matazamio makubwa ya kukutana naye Papa Francisco. Watu wazima wanakumbuka jinsi ilivyokuwa wakati walipotembelewa na Papa Mtakatifu Yohana Paulo II aliyetembelea Korea mara mbili, mwaka 1984 na 1989. Na hivyo hii ni ziara ya tatu kwa Korea kupata bahati ya kutembelewa na Papa. Na wanatambua kwamba ziara hii ya Papa ina siri ya neema ya Mungu ya kipekee, na hivyo wanashukuru na kumsifu Bwana. Na wanatambua kwamba, neema hii waliyopata inatokana na mafanikio ya historia ya Kanisa nchini Korea. Na kwamba, wamekuwa wakifuatilia nyayo za Papa Francisco tangu mwanzo mwa utawala wake, na dhahiri wameonesha kwamba, si mpenda makuu, daima amekuwa karibu na watu wa kawaida na maskini na hasa wale waliotupwa pembezoni na jamii. Na hasa wamevutiwa na juhudi zake za kutembelea mataifa yenye kuwa na migogoro yenye kuleta uchungu mkali kwa jamii, daima kujaribu kuonyesha huruma na faraja yake kwa watu wenye mahitaji.

Askofu Kang aliendelea kutoa historia fupi ya Korea, akitaja mgawanyiko wa kuumiza wa tangu miaka 66 iliyopita, iliyotenganisha Korea Kaskazini na Korea ya Kusini. Na ameitaja vita ya mwaka 1950 iliyosababisha watu nusu ya milioni, kuuawa, na wengine zaidi milioni tatu , kubaki majeruhi. Na hadi sasa hakuna amani kati ya Korea hizi mbili, bado kuna wasiwasi za kutisha za mapigano. Hivyo Pande zote mbili zimejiweka tayari kwa vita wakati wowote, kila upande ukiwa umejiimarisha kijeshi hasa katika kutengeneza silaha za kisasa zaidi.

Na alionyesha masikitiko yake kwamba, kuna kundi kubwa la watu walio lazimishwa kutengana na Familia zao. Wale ambao wanaishi eneo la Kaskazini wanalazimishwa kujitenga na wanaoishi eneo la Kusini, sasa yafikia miaka 66, ingawa ni watu wa mbali moja na hutumia lugha moja, lakini wamekuwa wakiishi chini ya mifumo tofauti ya kisiasa, kiitikadi na hali tofauti kiuchumi, licha kuwa utamaduni wao asilia wafanana. Pamoja na hayo yote, tatizo kubwa, ni jinsi ya kufikia muafaka wa dhati kati ya ndugu hawa wa Kaskazini na Kusini, watu ambao ni kaka na dada na jirani.

Askofu Kang, Pamoja na kuzungumzia hali ngumu ya kisasa katika rasi hii ya Korea, pia alitazamisha katika kipindi cha zaidi ya nusu karne iliyopita, akisema jamii ya Korea imepiga hatua za haraka sana katika ukuzaji wa viwanda, demokrasia na Uinjilishaji , kiasi cha kuwa mfano kwa nchi nyingine zinazoendelea. Lakini mabadiliko haya ya haraka, pia yamesababisha madhara mengi yaliyoacha majeraha makubwa yasiyo ponyeka kirahisi, hasa kutokana na mfumo huria wa kiuchumi ambao umepanua pengo kati ya matajiri na maskini. Watu wana mateso mengi, hasa kutokana na wasiwasi wa kazi na ukosefu wa usalama wa kijamii, ambao umesababisha matukio mengi ya watu kujiua. Na ni kweli kwamba, kanisa limekua haraka katika muda mfupi, lakini Maaskofu wanautazama ukuaji huu, hasa wakionyesha kujali kiwango cha imani tangu kwao wenyewe na jamii kwa ujumla na kuona kwamba, bado jamii ya Wakristo inahitaji kujengwa katika misingi ya kweli ya Kiinjili.

Na hivyo, Askofu Kang alimkaribisha Papa kwa kusema Watu wa Korea wanahitaji faraja na kutiwa moyo na Baba Mtakatifu. Watu wa Korea, wanahitaji sana kujenga umoja na maelewano miongoni mwao, Watu wote kutoka Asia ya Kaskazini, wanahitaji kupewa matumaini kwa ajili ya amani. Na hivyo wameweka matumaini yao kwa baraka za ujio wa Papa Francisco katika rasi ya Korea. Alieleza na kumalizia kwa kuomba baraka za Papa kwa ajili ya Nchi ya Korea , hasa katika utambuzi wa kuwa na tumaini la kweli kwa watu mbalimbali wa Asia. Na alimshukuru tena Papa kwa kukubali mwaliko wao kwa hiari wa kuitembelea Korea.
Asante sana!








All the contents on this site are copyrighted ©.