Jubilee ya miaka 25 ya Masista wa Mitundu, Tanzania
Shirika la Masista wa Pendo wa Huruma wa Mtakatifu Vinsenti wa Paolo Mitundu, Tanzania
linaadhimisha Jubilee ya miaka 25 tangu Shirika hili lilipoingia nchini Tanzania kutoka
Austria. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 15 Agosti 2014 kwa Ibada ya Misa Takatifu
inayotarajiwa kuongozwa na Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba na Msimamizi
wa Kitume wa Jimbo Katoliki Singida. Ifuatayo ni historia fupi ya pilika pilika za
kuanzishwa kwa Shirika hili nchini Tanzania. Uwepo wa Shirika letu hapa Mitundu
-Tanzania ni tunda la Upendo wa Masista wa Pendo la Huruma wa Mt. Vinsenti wa Paulo
wa Innsbruck. Hatua zake Shirika letu lilianza kama Mission ndogo baada
ya kuwasili Tanzania Masista wetu waasisi:, Sr. Celine Mittelberger na Sr. M. Relinde
Kleber Novemba, mwaka 1981, Sr. M. Carmen Saxl mwaka 1982 na baadaye Sr. Waltraud
Mahlknecht mwaka 1983, kwa lengo la kufanya kazi ya umisionari kwa kutoa huduma za
jamii kama vile afya, huduma ya mama na mtoto na elimu bila kufundisha watu Habari
Njema ya Ufalme wa Mungu kwa njia ya katekesi na mafundisho mengine ya dini.
Historia
yatuambia kwamba mnamo mwaka Mwaka 1981 Sr. M. Carmen pamoja na Sr. M. Corona walifika
Tanzania sehemu ya Puma kwa ombi la Sr. Maria Mama Mkuu wa Shirika la Bikira Maria
Malkia wa Ulimwengu kwa ajili ya kuwafundisha wasichana namna ya kuwahudumia wagonjwa
na akina mama wajawazito. Lakini waliona hapo siyo mahali pao. Kwa hiyo walihitaji
kuondoka ili kurudi Ulaya. Lakini walipofika Arusha walikuatana na Padre Dominiko
wa Jamii ya wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu akawapeleka Heka kuwaonesha mahali ambapo
wangeweza kutoa huduma. Lakini hata hapo haikuwezekana.
Baada ya kurudi Ulaya
Mapadre wa Damu Azizi ya Yesu chini ya uongozi na Padre Mario Dariozzi waliwaalika
Masista wa Pendo la Huruma wa Mt. Vinsenti wa Paulo wa Innsbruck kufika kutoa huduma
za kijamii katika moja ya Parokia ambazo wanatoa huduma katika Jimbo la Singida.
Ndipo Sr. M. Carmen akifuatana na Sr. Alexia, Bwana Bernado Duelli na mafundi waashi
wawili kutoka Italia aliwasili Tanzania ili kuanza Umisionari.
Tarehe 17/01/1982
walifika Parokia ya Itigi wakapokelewa na Padre Francesco Paroko wa wakati huo. Tarehe
19/01/1982 waliwasili Mitundu kuona eneo lao kwa mara ya kwanza na kuamua kujenga
nyumba kwa ajili ya huduma walizokusudia kuzitoa.
Penye nia pana njia: Pamoja
na kwamba mwanzo ulikuwa mgumu sana, Masista waasisi walimtegemea Mungu katika yote
kama Abrahamu alivyomtegemea Mungu bila kujua itakuwaje mbele ya safari yake. Wao
pia walianza kazi yao bila kujua itakuwaje baadaye. Walikumbana na changamoto mbalimbali
kama vile:
Kutokuwa na nyumba ya kulala. Kupika chini ya mti.
Kusafiri kila siku kurudi Itigi baada ya kazi ingawa miundo mbinu ilikuwa duni. Kutoa
huduma za afya kwa ajili ya wagojwa, wajawazito,na watoto kwenye Kanisa dogo la kigango
na katika majumba ya watu. Ujenzi wa shida kutokana na uhaba wa maji, ukosefu wa
vifaa kama gari kwa ajili ya kubeba mchanga, mawe, vifaa vya ujenzi na mengineyo.
Pamoja
na ugumu huu walifanikiwa kumaliza nyumba moja. Wakiwa wanaendelea na ujenzi walikabiliwa
na tatizo la ukosefu wa gari kwa ajili ya kubeba mchanga na vifaa vingine vya ujenzi.
Waliomba msaada kwa Hayati Mhashamu Askofu Benard Mabula wa Jimbo Katoliki Singida
naye akawasaidia, (Raha ya milele umpe ee Bwana …. Astarehe kwa amani. Amina). Kutoka
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida waliazima mashine ya kuchomelea vyuma na hatimaye
walifanikiwa kuezeka nyumba ya pili. Wanasimulia kwamba, siku inayofuata mvua kubwa
ilinyeesha (1983) na hapo walionja kwa namna ya pekee upendo wa Mungu, walitambua
mapenzi ya Mungu kwao, kama asemavyo Mtakatifu Vinsenti wa Paulo: “Mambo ya Mungu
huja yenyewe na hekima ya kweli ipo katika kufuata Maongozi ya Mungu hatua kwa hatua”.
Taabu
na mahangaiko havikukomea hapo. Siku moja Sr. M. Carmen akiwa safarini toka Itigi
aliharibikiwa na gari, akalazimika kutembea km zaidi ya 16 kwa miguu kutoka Kijiji
cha Itagata hadi Mitundu akiwa amembeba Yesu wa Ekaristi Takatifu mikononi.
Masista
waliendelea na ujenzi huku wakitoa huduma. Ili kuweza kutoa huduma ya mapendo kwa
Mungu na jirani kwa ufanisi walihitajika wasaidizi wengine. Ndipo tarehe 19/03/1985
kwa Maongozi ya Mungu aliwasili Mitundu msichana wa kwanza aliyeitwa Maria Kitiku
kujiunga na Masista hawa. Siku hiyo hukumbukwa kama ishara ya neema ya Mungu - kuanzisha
Shirika, ingawa tangu mwanzo Masista hawakuwa na lengo la kuanzisha Shirika hapa Tanzania.
Tarehe 02/02/1986 msichana huyu alianza hatua ya Upostulanti. Tarehe
12/06/1987 Unovisi Tarehe 04/06/1989 Sr. Maria Kitiku alifunga Nadhiri zake za
Kwanza na huu ndio ulikuwa mwanzo wa Shirika letu hapa Tanzania ambalo mwaka 2014
huu linatimiza miaka 25 na Sr. Maria Kitiku anatimiza miaka 25 ya utawa katika Shirika
hili. Asante Sr. Maria Kitiku kuitika wito wa kuwa mhudumu wa maskini na kuwa nyota
ya matumaini katika Shirika letu hapa Tanzania. Nadhiri zake za Maisha alifunga
tarehe 17/06/1995.
Kama Mungu alivyomwambia Abrahamu: ‘‘Nitakufanya
kuwa Baba wa Mataifa mengi” Mwa 17: 4. Masista wetu pia kwa imani waliyokuwa nayo
kwa Mungu wamefanywa “MAMA” wa mataifa na makabila mengi. Tena jina lao si hilo tu
bali wameitwa pia ‘‘WAASISI‘‘. Kutoka mche mmoja mwaka 1989 mpaka sasa Shirika
letu hapa Tanzania lina jumla ya:
Masista wazalendo – 120: ambao
wanafanya utume katika majimbo manne nchini Tanzania: Singida: Mitundu, Itigi na
Kiyombo Dar es Salaam: Vikindu Mbeya: Lupa Tingatinga, Mwanjelwa na Mahenje. Kigoma:
sehemu ya Uvinza.
Wanovisi - 10 Wapostulanti- 13 Wakandidati-
21
Shirika letu halikuku a na kuongeza tu katika idadi ya wanachama
bali hata katika hadhi: Mwaka 1996 Mission ndogo ya Mitundu ilipewa hadhi ya kuwa
Region, wakati huo walikuwa Masista 18 jumla wazalendo pamoja na waasisi wetu. Mnamo
Julai 27, mwaka 2012 wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirika uliofanyika Makao Makuu ya
Shirika Innsbruck nchini Austria, Region ya Mitundu ilipewa hadhi ya kuwa Provinsi
ya Mitundu – Tanzania na kusimikwa rasmi hapa Tanzania tarehe 27/09/2013. HUDUMA
ZA SHIRIKA Masista wetu wamekuwa mstari wa mbele kuratibu na kusimamia shughuli
mbalimbali ambazo wameturithisha sisi pia. Shughuli hizo ni hizi zifuatazo:
Huduma za kiroho kama vile, kufundisha dini mashuleni, kufundisha watoto
wadogo, wakatukumeni, kutembelea jumuiya ndogondogo za Kikristo na kutoa ushauri.
Huduma za jamii hususan Afya na Elimu, kuhudumia makundi maalum ya Wazee,
Wajane, waathirika wa VVU, watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
SHUKRANI Tunawashukuru
waasisi wetu kwa kukubali mwito wa Mungu kufika kwetu na kutuletea Roho na Karama
ya Watakatifu Vinsenti wa Paulo na Luise wa Marillac. Asanteni Masista wetu kwa moyo
wenu wa majitoleo, kujituma kwenu, bidii na uvumilivu wenu. Jumuiya imekua na leo
tunashangilia, Jubilee oyee!
Tunawashukuru wakubwa wetu huko Innsbruck na Provinsi
zote za Ulaya na wafadhili mbalimbali kwa upendo wenu mnaotuonesha na kwa misaada
mbalimbali mnayotupatia.
Tunalishukuru Kanisa la Tanzania kuridhia uwepo wa
Shirika letu na kwa kuzitambua huduma zetu. Kwa namna ya pekee tunatoa shukrani za
pekee kwa Hayati Askofu Bernard Mabula kwa kuwapokea Waasisi wetu katika Jimbo la
Singida na kuwaruhusu kumsimika Mt. Vinsenti hapa Mitundu ili aendelee kutoa huduma
kwa wahitaji kupitia sisi Masista wake.
Tunamshukuru pia Mhashamu Askofu Desiderius
Rwoma, Mapadre, watawa na waamini wote wa Jimbo la Singida kwa ushirikiano uliopo.
Tunawiwa shukrani kwa ajili ya upendo na mchango mkubwa wa Wamisionari wa Shirika
la Damu Azizi ya Yesu katika kuanzishwa Shirika letu hapa Mitundu. Mungu azidi kuwabariki.
Tunawashukuru watu wote wa Mitundu na vijiji vya karibu kwa ujirani mwema.
Tunaishi kwa ushirikiano mzuri. Katika matukio ya furaha na huzuni tupo bega kwa bega.
Serikali ya Kijiji inatambua uwepo wetu na huduma tunazotoa. Tuendelee kushirikiana,
kupendana, kuthaminiana na kuheshimiana.
Mwisho tunamshukuru aliye mwanzo na
mwisho wa yote kwa kututunukia zawadi ya Shirika la Pendo la Huruma. Zawadi ambayo
ni mapenzi yake na tunda la Roho Mtakatifu anayeongoza Shirika letu kupitia wakubwa
wetu. Jambo la muhimu kwetu ni kutekeleza utume wetu tukiongozwa na neno la Baba
Vinsenti lisemalo: „Unipe mtu wa sala naye anaweza yote“. Sala inachukua nafasi ya
kwanza Malezi, kazi na kujituma ni jukumu letu wote wanavinsenti ili kuitunza vizuri
zawadi yetu. MUNGU LIBARIKI SHIRIKA LETU.