2014-08-13 09:19:54

Wekezeni katika familia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu!


Familia ni rasilimali muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa Mwaka 2015. RealAudioMP3

Hii ina maana kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika kuibua mbinu na mikakati itakayoiwezesha Familia kutekeleza dhamana na wajibu wake katika ustawi na maendeleo ya mwanadamu. Serikali, Mashirika ya kimataifa, taasisi na vyama vya kiraia havina budi kuzisaidia familia katika kufanikisha malengo haya.

Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, majadiliano mengi yanayoendelea kutolewa na wadau mbali mbali yanaonesha kana kwamba, Familia ni kikwazo kikuu cha ustawi na maendeleo ya mwanadamu. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kutokana na mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na ongezeko la idadi ya watu duniani, familia zinajikuta zikishindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa msingi.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva akichangia katika mkutano wa ishirini na sita wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, ujumbe wa Vatican unakazia umuhimu wa Familia katika maisha ya kijamii licha ya changamoto, magumu na kinzani zilizopita na hata zile ambazo zinaiandama Familia katika ulimwengu mamboleo.

Kuna sera na mikakati inayotaka kuhatarisha uwepo na udumifu wa Familia kwa kukazia masuala binafsi, uhuru usiokuwa na mipaka wala kujali kanuni maadili na utu wema, usawa unaotaka kufuta tofauti za msingi kati ya bwana na bibi pamoja na baadhi ya watu kuendekeza mno anasa na kusahau wajibu msingi wa Familia.

Familia na Jamii ni chanda na pete, ni mambo makuu mawili yanayotegemeana na kamwe hayawezi kutenganishwa, kiasi kwamba, kwa pamoja zinaweza kulinda na kukuza mafao ya binadamu wote. Haki binafsi zisiharibu tunu msingi za Familia na badala yake, watu wajielekeze zaidi katika kulinda na kutetea tunu msingi za kifamilia, kwa kuheshimu haki za mtoto katika familia, ili aweze kuishi na kutunzwa katika mazingira yatakayosaidia kukua na kukomaa kwa mtoto huyu kwa kuzingatia mifano inayotolewa na wazazi wake yaani: Baba na Mama.

Askofu mkuu Silvano Tomasi anasema familia ni nguzo muhimu katika Jamii inayoviwezesha vizazi kukutana, kupendana, kuelimishana, kusaidiana na kurithishana zawadi ya maisha. Hapa ni mahali ambapo wanafamilia katika utofauti wao wanajifunza kutegemeana kama inavyojionesha katika tamaduni na mapokeo mbali mbali ya binadamu.

Hii ni Familia inayojengwa katika mahusiano ya dhati kati ya Bwana na Bibi, wenye haki na wajibu; watu wanaoridhia mahusiano haya kwa utashi kamili pasi na shuruti. Kutokana na mwelekeo huu, kuna haja kwa Jamii kulinda na kutunza Familia.

Kwa mara nyingine tena ujumbe wa Vatican una penda kukazia kwamba, Familia haina budi kuimarishwa katika umoja na kamwe isigawanywe wala kubezwa. Ndoa na Familia ni tunu ambazo zinapaswa kulindwa na kutetewa si tu na Serikali bali na Jamii nzima. Kwa kushirikiana, Familia zinaweza kukabiliana na changamoto pamoja na magumu mbali mbali yanayojitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Haki msingi za binadamu hazina budi kutekelezwa pamoja na kuzingatia itifaki zilizoridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa zinazonesha haki, wajibu na tunu msingi zinazopaswa kuendelezwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.