2014-08-13 16:02:00

Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho!


Mpendwa mwana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho. Ni zawadi kwa Mama Bikira Maria anayokabidhiwa mwishoni mwa maisha yake hapa duniani. RealAudioMP3

Sherehe hii huja kila tarehe 15 ya mwezi wa nane kadiri ya kalenda ya kilturujia ya Kanisa Katoliki. Tunaposherehekea kupalizwa mbinguni kwa Mama Bikira Maria tunashangilia, lakini pia tunataka kukua katika imani katoliki ambapo tunakumbuka kuwa mama kanisa mnamo Novemba 1, 1950 katika mamlaka aliyokabidhiwa na Kristu, Baba Mtakatifu Pio XII katika ile hati iitwayo Munificentissimus Deus, ambayo tunaweza kuitafsiri kama “Mungu Mkarimu” alifundisha wazi na kwa milele kuwa Mama Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili ili amzae Mwana wa Mungu, aliyempa Yesu Kristu damu yake ya kibinadamu, akaambatana naye mpaka chini ya msalaba, amepalizwa mbinguni mwili na roho. Amepalizwa mbinguni mwili na roho ikiwa ni tuzo toka kwa Bwana wetu Yesu Kristu.

Fundisho hili la kupalizwa mbinguni mwili na roho, limefundishwa baada ya tafakari kina, kanisa likinyanyua maombi yake kwa Mungu, kwa njia ya Roho Mtakatifu wa ukweli, katika unyenyekevu na udumifu na hivi ikafunuliwa wazi na Mungu mwenyewe kuwa Bikira Maria amepalizwa mbinguni. Mpendwa msikilizaji, ni zawadi kwa kanisa, ni zawadi kwa kila mmoja wetu na hivi kinachofuata baada ya kupokea zawadi hii ya imani, ni heri na vigelegele kwa kwa kanisa takatifu mbele ya Mama Bikira Maria mtukuka aliye pia Mama wa Kanisa.

Mpendwa mwana wa Mungu, kwa sherehe hii tunafurahia kushirikishwa kwa Mama Bikira Maria katika utukufu wa mwanae Yesu Kristu Mkombozi pekee wa ulimwengu. Utukufu ambao mama huyu ameushiriki tangu mwanzo kwa fumbo la umwilisho, yaani Yesu Kristu kutwaa mwili wa kibinadamu kwa njia yake. Si hilo tu bali kupalizwa mbinguni kunaambatana na fumbo la pasaka na hivi Bikira Maria anamsindikiza mwanae mpaka chini ya msalaba akishuhudia mateso. Kwa namna hiyo basi Mwana asingeweza kumwacha mamaye aoze kaburini, lazima amtuze zawadi hiyo ya kupalizwa mbinguni. Kumbe Kanisa linapiga vigelegele kwa sababu ya kutukuzwa kwa Mama wa Mungu lililo tunda la ufufuko.

Katika kusherehekea kupalizwa mbinguni kwa mama Bikira Maria yafaa kutambua na kujifunza kidogo upi ni mzizi wa Bikira Maria kupalizwa mbinguni. Ndiyo kusema tangu mwanzo Mungu aliweka jambo hili katika mpango mathubuti. Tunaona katika kitabu cha Mwanzo, lile anguko la wazazi wa kwanza yaani Adamu na Eva, ambao kwa njia yao kifo kinaingia duniani, na mara moja tangazo la upendo toka kwa Mungu linatolewa kwa mwanadamu, likiwa ni kandamizo kwa shetani kama tusomavyo “nitaweka uadui kati yako wewe na huyo mwanamke” Mw 3:15 yaani nyoka aliyeleta anguko kwa wazazi wa kwanza anaambiwa atawekewa uadui mkali na uadui huu utakuja kwa njia ya mwanamke.

Kwa vyovyote vile mwanamke huyu asingeweza kuwa Eva kwa maana Eva na nyoka walifanya urafiki. Ni lazima awe mwanamke mpya kabisa. Mwanamke huyu kadiri ya mafundisho ya mababu na walimu wa Kanisa ni Mama Bikira Maria, ni Eva mpya, ni yule ambaye wokovu utaingia duniani kwa njia ya utii wake wake kwa Mungu. Kumbuka maneno yake kwa malaika Gabrieli akisema, “nitendewe kama ulivyonena” Na zaidi ya hilo uzao wake haiwezekani ukawa ni Adamu bali ni Adamu mpya, na hivi Yesu Kristu Masiya atakayetangaza uadui dhidi ya kifo yaani utawala wa shetani.

Kristu mshindi wa kifo, aliye Adamu mpya haachi kumshirikisha mama kwa karibu katika vita dhidi ya kifo na kwa namna hiyo basi Yesu na Maria wako pamoja katika uadui dhidi ya nyoka kielelezo cha mwovu shetani. Bikira Maria ni mkombozi mwenza (co- redemptoris) na hivi kwa sababu Mkombozi Yesu Kristu anapokufa mara moja kifo chake kinafuatwa na ufufuko, vivyohivyo mkombozi mwenza Mama Bikira Maria anapokufa lazima kifo chake kifuatwe mapema iwezekanavyo na ufufuko kabla ya ufufuko wa wote na hapa ndipo kuna kupalizwa mbinguni. Mantiki hii inakuzwa na mababu na walimu wa Kanisa wakianzia pale katika Proto – evangelium kitabu cha Mwanzo sura ya 3 :aya ya 15, Kama tulivyokwisha sema hapo mwanzoni.

Katika Agano Jipya, Bikira Maria anapokea salaam ya pekee toka kwa malaika Gabriel akimwambia “salaam Maria ewe uliyebarikiwa na Mungu! Bwana yuko nawe” Lk 1:28. Salaam hii ni amkio la juu kabisa (par excellence) lenye kuonesha kuwa tangu mwanzo wa maisha yake na hata mwisho hana doa la dhambi. Na hivi hayuko chini ya utawala wa kifo kilicho tabia ya dhambi. Ni mkingiwa dhambi ya asili na hivi kwa namna yoyote angepalizwa mbinguni mwili na roho.

Anaambiwa umebarikiwa kuliko na kati ya wanawake wote, kumbe baraka yake haichangamani na baraka za wengine. Baraka hii haiji tu bali anapewa kwa sababu amejaa neema tangu kuumbwa kwake na kwa sababu hiyo uwepo wa Bwana ni mkamilifu katika yeye. Baraka aliyonayo mama Bikira Maria ni kinyume na laana ya kale ya kurudi mavumbini kwa wazazi wetu wa kwanza. Mw 3:19. Ndiyo kusema kama Kristu ni mshindi dhidi ya kifo kilicholetwa na Adamu, basi Maria ni mshindi dhidi ya kifo kilicholetwa na Eva.

Kwa ushindi huu lazima Bikira huyu atuzwe zawadi ya kushiriki utukufu wa Mwanae kabla ya wanadamu wengine wote, ndiyo kupalizwa mbinguni. Kupalizwa Mbinguni ni kuendeleza ushindi na ni mlango wa kumfuasa Kristu kuingia mbinguni kwetu sisi tuliokabidhiwa kwake pale chini ya msalaba. “mama tazama huyu ndiye mwanao”! Kamwe mama hatatuacha katika uvuli wa machozi, lazima atatoa chozi la upendo kwa mwanae na tutapata ondolea na msamaha wa dhambi.

Nani kama mama? Mpendwa unayenisikiliza, kwa kupalizwa kwa Mama Bikira Maria mbinguni tunaona ujio wa shime kwa akina mama wote, na hivi tunashangilia nafasi kubwa katika maisha ya akina mama wanayozawadiwa kwa ushindi wa Maria mama mtukuka, tunda la kwanza la ukombozi.ni ushindi wa akina mama wote, ni ushindi wa familia zote.

Mpendwa mwana Kanisa tunapoadhimisha sherehe hii tunawaombea watawa wote wa mashirika mbalimbali waliojiweka chini ya ulinzi wa Bikira Maria mpalizwa mbinguni. Washike imani katoliki, wampende mama Maria kwa heshima na uchaji wa juu na zaidi wakue katika fumbo na fundisho hili la kupalizwa Mbinguni mama Bikira Maria.

Kwa namna ya pekee tunaalikwa pia kuwaombea Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu ambao tarehe hii ya 15 mwezi wa nane 1815 Shirika lao lilianzishwa na Mtakatifu Gaspari na kuwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria wa Damu Takatifu. Wamisionari hawa wanafanya kazi katika mabara ya Amerika, Ulaya, Asia na zaidi sana Afrika katika nchi ya Tanzania na Guinea Bissau. Wajibu na karama ni kutangaza upendo wa Damu Takatifu ya Kristu iliyotolewa msalabani kwa ukombozi wa ulimwengu.
Ninakusindikizeni kwa tafakari hii nikikuombea baraka tele za Bwana katika maisha yako zinazomwagika na kububujika kwa njia ya Bikira Maria mpalizwa Mbinguni, mama mtukuka juu ya wanawake wote, malkia wa mbinguni. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa Kwenu na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.