2014-08-13 09:30:15

Maisha ya kitawa na changamoto zake!


Kardinali Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume hivi karibuni akizungumza na wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume mjini Melbourne, nchini Australia amewataka watawa kujenga na kudumisha mahusiano yanayojikita katika vinasaba vinavyodhihirisha kwamba, Mungu ni upendo. RealAudioMP3

Wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, walikuwa wanafanya mkutano wao mkuu uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “ Kuishi changamoto wadau katika hali ya mabadiliko”.

Kardinali Braz anasema, leo hii haitoshi kuwa na kanuni maadili, urithi wa maisha ya kiroho kutoka kwa waanzilishi wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume au sera na mikakati ya kichungaji inayowawezesha watawa kutangaza kwa ari na moyo mkuu Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Kumbe, kuna haja kuonesha ushuhuda wa maisha ya kitawa unaojikita katika maisha ya pamoja yanayokuza na kudumisha tasaufi ya umoja, upendo na mshikamano, mambo msingi aliyokazia Mtakatifu Yohane Paulo II kama nguvu ya Kanisa, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Watawa wanapaswa kujibu changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wao katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kujikita katika utekelezaji wa mwaliko unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa watawa kuhakikisha kwamba, wanauamsha ulimwengu, na huu ukawa ni mwanzo wa cheche za maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Kardinali Braz anasema, nyakati hizi kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mambo ambayo yamelea mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadamu katika medani mbali mbali za maisha. Mahusiano na mwingiliano kati ya watu ni mambo yanayokwenda kwa haraka na kwa nguvu ya ajabu hata na wale ambao wako mbali kabisa.

Leo hii maendeleo ya mitandao ya kijamii yanawawezesha watu kupata habari za haraka kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, ulimwengu mamboleo umekuwa kama kijiji! Watu wanaweza kusafiri kwenda sehemu mbali mbali za dunia kwa kutumia muda kidogo, yote haya yanaonesha jinsi ambavyo utandawazi ulivyokuwa na kukomaa.

Lakini, changamoto kubwa kwa sasa ni kuona kwamba, zile tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zilizowaunganisha watu kutoka kila kabila, lugha, jamaa na taifa zinawekwa pembeni kana kwamba, zimepitwa na wakati. Hizi ni tunu msingi za maisha ya mwanadamu zilizojenga na kukuza mahusiano kati ya mwanadamu na Muumba wake na kati ya binadamu wenyewe, leo hii, ubinafsi, dhana ya mawazo mepesi mepesi na watu kumezwa na malimwengu, ni mambo yanayoendelea kumkoroga mwanadamu.

Bila uwepo wa Mwenyezi Mungu, Sheria na Kanuni maadili, kila mtu anakuwa ni hakimu wa mawazo na matendo yake; anakuwa na uwezo wa kujitafuta mwenyewe na kuambatana na mambo yanayompatia furaha hata kama ni furaha ya mpito. Tunu msingi za maisha na ukweli wa binadamu zinawekwa rehani, kiasi cha kuvuruga mahusiano kati ya watu.

Kardinali Braz anasema, kwa mtindo na mwelekeo huu wa mawazo, nadhiri ya utii, ufukara na usafi kamili zinaonekana kuwa ni mambo ya kale, yaliyopitwa na wakati, eti watu wanapaswa kuponda mali, kufa kwaja! Hapa umuhimu wa maisha ya pamoja, unaangaliwa kwa jicho la kengeza, kwani kwa hapa wanasema, maisha ya kijumuiya ni mateso makubwa kwa mtawa.

Ukweli huu unajionesha hata miongoni mwa watawa walioweka nadhiri za daima na wale ambao wameanza kuchungulia tu maisha ya kitawa kwa kutaka kuachana kidogo na maisha haya, ili waonje kile ambacho wamekikosa huko duniani, kwa maneno mengine ni watu wanaotaka kuonja uhuru binafsi na wasipokuwa makini, huko wanajichumia majanga!

Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linasema, sababu kubwa inayotolewa na watawa wanaotaka kuacha maisha ya kitawa si kwamba, walikosea kuchagua wito, bali ni kutokana na hali ya kutosikia tena Jumuiya yao ya kitawa kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, hapa Jumuiya imekuwa kama ni gereza dogo, mahali ambapo mtu anashindwa kujiamria mambo yake mwenyewe, kimsingi, watawa hawajisikii kamwe kwamba, wana ile furaha waliyokuwa nayo siku ile walipokuwa wanapigiwa vigelegele na kuvikwa mashada ya maua kwa kuweka nadhiri zao za daima!

Hali na mwelekeo huu ni changamoto kubwa kwa watawa na inahitaji watawa wenyewe kujenga na kuimarisha mahusiano yao yanayojikita kwa kutambua kwamba Mungu ni upendo n ani chanzo mshikamano wa upendo kati ya watu wanaotoka katika kila kabila, lugha na jamaa. Ni watu ambao wamekombolewa kwa Damu ya Mwanakondoo wa Mungu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.