Kituo cha Radio Kabangabanga Zambia chazinduliwa rasmi!
Askofu mkuu Julio Murat, Balozi wa Vatican nchini Zambia, hivi karibuni alizindua
Kituo Kipya cha Radio Katoliki Kabangabanga, kilichopo Jimboni Solwezi, Zambia. Askofu
Charles Kasonde wa Jimbo Katoliki Solwezi ndiye aliyebariki kituo hiki ambacho kinakuwa
ni kituo cha tisa cha Radio zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini
Zambia.
Serikali ya Zambia imelipongeza Kanisa kwa kuanzisha kituo cha radio
na kuwataka kuhakikisha kwamba, wanatengeneza vipindi kadiri ya mahitaji ya wananchi
wa Zambia, hasa kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, maadili na
utu wema, mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika tasnia ya habari.
Takwimu
zinaonesha kwamba, walau kila Jimbo Katoliki nchini Zambia, limebahatika kuwa na Kituo
cha Radio kama sehemu za utekelezaji wa mikakati yake ya shughuli za kichungaji, zinazopania
Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kwa kutimia njia za mawasiliano
ya kisasa. Itakumbukwa kwamba, kuibuka na kuenea kwa Vituo vya Radio vinavyomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa Katoliki ni matunda ya maadhimisho ya Awamu ya kwanza ya Sinodi
ya Maaskofu wa Bara la Afrika, iliyofanyika mjini Vatican kunako mwaka 1994.
Hadi
sasa nchini Zambia, kuna vituo viwili vya radio ambavyo vinafanyiwa kazi kwa sasa
navyo ni Radio Lutanda kilichoko Jimbo kuu la Kasama na Kituo cha radio Sesheke, kitakachokuwa
Magharibi wa Jimbo la Sesheke.