Baba Mtakatifu Francisko anapoianza hija yake ya kitume nchini Korea ya Kusini inayoongozwa
na kauli mbiu "Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia"
anawaalika Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana naye kwa njia ya sala
ili kuiombea Korea na Asia katika ujumla wake.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu
mkuu wa Vatican anasema hija ya kitume ya Baba Mtakatifu ina umuhimu wake kwa maisha
na utume wa Kanisa Barani Asia. Kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu anafanya hija ya
kitume Korea ya Kusini, lakini akiwa na mwelekeo kwa Kanisa zima Barani Asia, kwani
Baba Mtakatifu atashiriki katika maadhimisho ya Siku ya Sika ya Vijana Barani Asia.
Lakini, ikumbukwe kwamba, Bara la Asia linaendelea kuimarika katika masuala
ya kisiasa na kiuchumi. Baba Mtakatifu anapenda kuwekeza kwa vijana Barani Asia, ili
waweze kuwajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wanapaswa kuwa
ni Wainjilishaji miongoni mwa vijana wenzao, kwa kujikita katika majiundo makini yanayozingatia
ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu akiwa nchini Korea anatarajia
kuwatangaza Wafiadini 124 kutoka Korea ya Kusini kuwa ni Wenyeheri. Hili kundi kubwa
la waamini walei na kati yao kuna Padre mmoja tu; waamini ambao walijisadaka kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini Korea, changamoto kwa waamini walei kuwa kweli
ni mashahidi wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanahamasishwa kuwa ni watangazaji
wa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha; kwa kuchuchumilia utakatifu
wa maisha kadiri ya wito na nafasi ya kila mwamini.
Akiwa nchini Korea, Baba
Mtakatifu atakutana na kuzungumza na watu walioguswa na ajali ya kuzama kwa Meli huko
Sewol, na kusababisha watu 300 kupoteza maisha yao. Hii ni ajali ambayo imewagawa
wananchi wa Korea ya Kusini. Baba Mtakatifu anataka kuonesha jinsi ya kuponya madonda
ya ndani, kwa kuwa karibu na wote walioguswa na ajali hii mbaya; hiki ni kielelezo
cha imani na upendo.
Kardinali Parolin anasema, Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha
hija yake ya kitume kwa kusali kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho kati ya Korea
ya Kusini na Korea ya Kaskazini, kwani Korea bado inaendelea kuteseka kutokana na
uwepo wa vita baridi, ambayo kwa sasa haina tena mashiko wala mafao kwa ustawi na
maendeleo ya watu. Vatican inapenda kushiriki katika mchakato wa majadiliano, ili
kujenga na kuimarisha upatanisho na umoja wa kitaifa.