2014-08-13 09:09:58

Furaha ya kimissionari!


Furaha ya Injili inajikita katika maisha na utume wa kimissionari, ndiyo kauli mbiu itakayofanyiwa kazi na wajumbe wa mashirika na vyama vya kitume, wakati wa maadhimisho ya Kongamano la tatu la kimissionari kimataifa, litakalofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 22 Novemba 2014. RealAudioMP3

Huu utakuwa ni wakati muafaka wa kufanya majadiliano ya kina na viongozi mbali mbali kutoka Vatican. Hadi sasa kuna zaidi ya wakuu wa mashirika na vyama vya kitume 55 na vyama 80 kutoka sehemu mbali mbali za dunia vimeridhia kushiriki katika kongamano hili la kimataifa.

Itakumbukwa kwamba, Kongamano la kwanza la mashirika na vyama vya kitume lilitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1998 na awamu ya pili kunako mwaka 2006 na wajumbe wakapata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste kwa mwaka 2013 katika Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa mashirika na vyama vya kitume ndani ya Kanisa.

Wajumbe wa vyama hivi walikumbushwa kwamba, wao ni zawadi kubwa na utajiri wa Roho Mtakatifu kwa Kanisa, changamoto ya kuendeleza mbele nguvu ya Injili, ili iweze kugusa undani wa maisha ya watu, pasi na kuwa na woga wala makunyanzi, daima wakiwa ni watu wenye furaha ambao wameungana na Kristo pamoja na Kanisa lake.

Hii ni changamoto kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa kuwatangazia watu Injili ya Furaha inayojikita katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha, wakati huu Mama Kanisa anapojielekeza zaidi na zaidi katika Uinjilishaji Mpya.

Kongamano hili litakuwa ni fursa nyingine kwa mashirika na vyama vya kitume ndani ya Kanisa kutafakari ili hatimaye, kuweza kumwilisha changamoto za kichungaji zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa, kama sehemu ya matunda ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, umri wa mtu mzima kabisa!

Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hili, ili kwa pamoja, waweze kuonesha ile furaha ya kujikita katika maisha na utume wa kimissionari, tayari kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei ndilo lenye dhamana ya kuratibu na kuwezesha maadhimisho ya kongamano hili la kimataifa na kwamba, hadi sasa viongozi wa kuu wa Baraza hili wanayashukuru mashirika na vyama vya kitume ambavyo vimeonesha nia ya kushiriki katika maadhimisho ya kongamano hili, ili kwa pamoja waweze kujifunga kibwebwe kutembea kwa pamoja, kujenga Kanisa la Kristo, kwa kujikita katika maisha na utume wa Kimissionari.

Lengo ni kuendeleza majadiliano kati ya Kanisa na ulimwengu, kati ya Kanisa na tamaduni mbali mbali zinazomzunguka mwanadamu wa leo. Changamoto kubwa hapa ni kuamsha ari na mwamko wa kimissionari unaojikita katika toba na wongofu wa ndani; mambo msingi katika maisha ya mtu binafsi na kwa ajili ya Familia yote ya Mungu.

Umoja na mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa ni mambo msingi yanayoyawezesha Mashirika na vyama vya kitume kutekeleza wajibu na dhamana yao ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya kongamano hili la kimataifa yatajielekeza kwa kuwapatia wajumbe fursa ya kukutana, kujadiliana na kushirikishana maamuzi na vipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.