2014-08-13 12:02:31

Barua ya Papa kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Iraq


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe maalum Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon kumwelezea hofu na mashaka yake kuhusu mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia Kaskazini mwa Iraq, wengi wao wakiwa ni Wakristo wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa nyumba za ibada na urithi wa kidini.

Kwa kusukumwa na mateso ya watu hawa, Baba Mtakatifu anasema amemtuma kama mjumbe wake maalum nchini Iraq, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Vatican nchini Iraq, ili kuonesha mshikamano wake wa dhati na Kanisa zima, kwa watu wanaotaka kuishi kwa amani, utulivu na uhuru katika ardhi ya Mababu zao.

Baba Mtakatifu anasema, anamwandikia ujumbe huu Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, akiweka mbele yake machozi, mahangaiko na hali ya kukata tamaa inayooneshwa na Wakristo pamoja na makundi madogo madogo ya kidini nchini Iraq. Anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha majanga haya.

Baba Mtakatifu anayahimiza Mashirika ya Kimataifa hususan yanayojihusisha na masuala ya usalama, amani, sheria na huduma kwa wakimbizi, kuendeleza juhudi zao kadiri ya Sheria za Umoja wa Mataifa. Mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia Kaskazini mwa Iraq yaamshe dhamiri nyofu kwa watu wenye mapenzi mema ili kuonesha mshikamano wa upendo kwa kuwalinda waathirika pamoja na kuwapatia msaada wanaohitaji wale wote wasiokuwa na makazi maalum kwa wakati huu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanafanikiwa kurudi katika makazi yao salama salimini.

Kuna haja ya kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kwa kuzingatia sheria za kimataifa pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaweka mikakati makini itakayozuia mauaji yanayojikita katika ukabila na udini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko na Wakuu wa Makanisa ya Mashariki pamoja na viongozi mbali mbali kwamba, ujumbe wake utapata jibu makini kutoka katika Umoja wa Mataifa.









All the contents on this site are copyrighted ©.