2014-08-12 08:52:52

Pasi na Ukristo Mashariki ya Kati ni kutumbukia katika umaskini mkubwa!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss anasema kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwalinda Wakristo wanaoshambuliwa kwa sasa nchini Iraq, kiasi cha kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia.

Hili ni kundi ambalo kwa sasa linakabiliwa na uhaba wa maji na chakula na watu wengi wameanza kuchoka na kupoteza maisha wakiwa njiani kukimbia vita. Mashambulizi yanayofanywa na Serikali ya Marekani yanayoungwa mkono na nchi marafiki ni muhimu ili kuwalinda watu wanaolazimika kuikimbia nchi yao, lakini zaidi kuna haja ya kuwashughulikia kimataifa wale wote wanaowauzia silaha na kuwafadhili kwa njia ya rasilimali fedha.

Nchi ambazo zinaunga mkono vita ya jihadi zinapaswa kusitisha mwelekeo huo, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Iraq, wawe waamini wa dini ya Kiislam au Wakristo, vita ni chanzo kikuu cha uharibifu na maafa kwa watu. Machafuko yanayoendelea nchini Iraq ni mwendelezo wa majanga yanayojitokeza huko Mashariki ya Kati.

Jeshi la Jihadi linaendelea kufanya mauaji makubwa ya watu pasi na huruma, hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi na mafao ya wengi; hapa watu wasutwe na dhamiri zao nyofu kutokana na mateso ya watu wasiokuwa na hatia.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon analaani vikali mauaji dhidi ya Wakristo kwa kusema kwamba, hivi ni vitendo visivyokubalika. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni limejadili pia hali ya Makundi madogo madogo yanayotishiwa usalama wake huko Mashariki ya Kati na kwamba, hapa walengwa ni Wakristo. Huu ni uvunjifu wa haki msingi za binadamu.

Jambo la kutia moyo ni kuona kwamba, hata katibu mkuu wa Shirikisho la Nchi za Kiislam amelaani mauaji ya Wakristo na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kulinda haki zao msingi na kuendelea kuishi nchini Iraq kama raia wengine wa Iraq. Mashariki ya kati pasi na Ukristo ni kutumbukia katika umaskini mkubwa, kwani hata Uislam wenyewe utakosa msukumo wa demokrasia na majadiliano na sehemu nyingine ya dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.