Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaojisadaka
kwa ajili ya kuwasaidia maskini, wakati huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina
linapoadhimisha Siku ya 45 ya Sadaka kwa ajili ya Maskini, linaloongozwa na kauli
mbiu "Asante kwa msaada wako".
Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa
niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Adolfo
Armando Uriona, Mwenyekiti wa Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kwa ajili
ya msaada kwa maeneo yenye uhitaji zaidi, anawatia shime waamini kuonesha imani yao
kwa njia ya matendo ya kawaida kwa kutokumbatia mno malimwengu, ili kuonesha mshikamano
wa upendo, ili waendelee kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa dunia kwa njia ya imani
tendaji; upendo wa kidugu na mshikamano wa dhati kwa maskini wanaoonesha ile sura
ya Kristo!
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na kwamba, anawaweka
wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mama yetu wa Lujan, ili tukio hili
la mshikamano liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa!