2014-08-12 10:15:44

Askofu mkuu Zaluski ni kielelezo cha amani na matumaini nchini Burundi


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 9 Agosti 2014 amemweka wakfu Askofu mkuu Wojciech Zaluski, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Lomza, nchini Poland.

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amemtaka Askofu mkuu Zaluski kusaidia mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya amani na matumaini nchini Burundi. Amemtaka awasilishe salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Burundi, ili kujenga na kuimarisha kifungo cha umoja na upendo kati ya Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu. Kipaumbele cha kwanza ni huduma kwa Familia ya Mungu nchini Burundi.

Kardinali Parolin amemtaka Askofu mkuu Zaluski kutekeleza dhamana na utume wake kwa unyenyekevu na uvumilivu; hekima na busara katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya amani na utulivu hatika katika mazingira ambayo bado ni tete, ili watu waweze kutambua kwamba, kwa kujikita katika utashi na kwa njia ya msaada wa Mwenyezi Mungu, watu wanaweza kuishi kwa amani, utulivu huku wakisaidiana kwa hali na mali.

Kardinali Parolin anakumbusha kwamba, Balozi wa Vatican katika nchi yoyote ile kimsingi ni mtu wa umoja na amani mintarafu wito wake. Ni kiungo muhimu kati ya Mungu na mwanadamu. Ni kiongozi anayeyakita maisha yake katika matumaini hasa pale anapokabiliana na hali ngumu ya maisha katika utume wake, kwani anatambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayeongoza historia ya maisha ya mwanadamu.

Ili Balozi wa Vatican aweze kutekeleza dhamana hii nyeti anapaswa kuwa kweli ni mtu wa Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Adhimisho la Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayomwilishwa katika huduma ya mapendo.

Kwa Askofu mkuu Wojciech, si mgeni sana nchini Burundi, kwani hapa ndipo alipoanzia utume wake kama Mwakilishi wa Baba Mtakatifu. Burundi ina utajiri mkubwa wa historia na tamaduni, lakini pia kwa miaka ya hivi karibuni imetikiswa na kupepetwa kama ngano kutokana na mauaji ya kimbari. Burundi inahitaji uponyaji wa ndani na ukuaji wa maisha ya Kikristo yanayotoa ushuhuda wa imani tendaji, kwa kuwa waaminifu kwa Injili ya Kristo.

Askofu mkuu Zaluski anapaswa kuwa kweli ni kielelezo cha amani na ukweli katika utekelezaji wa dhamana yake kama Mwakilishi wa Baba Mtakatifu nchini Burundi pamoja na kuendeleza mchakato wa umoja na upatanisho wa kitaifa unaojikita katika kumbu kumbu na mioyo ya wananchi.







All the contents on this site are copyrighted ©.