2014-08-11 10:54:07

Vita nchini Iraq inaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao!


Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 10 Agosti 2014, kwqenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza mawazo yake nchini Iraq ambako kuna maelfu ya watu wanaoendelea kuteseka na kati yao kuna idadi kubwa ya Wakristo ambao wamefukuzwa kutoka katika makazi yao; watoto wanaokufa kwa kiu na njaa barabarani; wanawake waliotekwa na kufanyiwa nyanyaso za kila aina; kuna uharibifu mkubwa wa makazi ya watu na makumbusho ya kidini, kihistoria na kitamaduni.

Baba Mtakatifu anasema, matukio yote haya yanamchukiza Mwenyezi Mungu na kumwathiri binadamu. Ni jambo ambalo halikubaliki kufanya vita kwa jina la Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu huko Iraq. Anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kusitisha mauaji haya ya kimbari na kuhakikisha kwamba, haki inatawala.

Baba Mtakatifu ameonesha masikitiko yake kutokana na kuanza tena kwa mashambulizi kwenye Ukanda wa Gaza baada ya mashambulizi haya kuwa yamesistishwa kwa muda. Baba Mtakatifu amewakumbuka pia watu walioathirika kutokana na ugonjwa wa Ebola na wale wote wanaoendelea kujitaabisha ili kuhakikisha kwamba, ugonjwa huu unadhibitiwa kikamilifu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika hija yake ya kichungaji nchini Korea ya Kusini, kuanzia Jumatano tarehe 13 hadi tarehe 18 Agosti 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.