2014-08-11 11:32:57

Ujumbe wa Papa Francisko kwa wananchi wa Korea!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa video ambao amewatumia wananchi wa Korea anawaambia kwamba, baada ya muda si mrefu atakuwa kati yao na kwamba, kuanzia wakati huu anapenda kuwashukuru kwa kumwonesha ukarimu na anawaalika kumwombea katika sala zao, ili hija hii ya kitume iweze kuzaa matunda bora kwa Kanisa na Jamii ya Korea.

Baba Mtakatifu anatumia maneno ya Nabii Isaya, Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Korea, kuupokea mwanga unaotoka kwa Kristo. Anawaalika vijana kutoka Barani Asia kuondoka na kusimama ili waweze kuangaziwa na utukufu wa Mashahidi, uliojionesha kwa namna ya pekee na Paul Yun Ji-Chung na wenzake 123, anaotarajia kuwatangaza kuwa Wenyeheri hapo tarehe 16 Agosti 2014, huko mjini Seoul.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, wao ni vyombo vya matumaini na nguvu mpya kwa kesho iliyo bora zaidi, lakini pia wahanga wa mmong'onyoko wa maadili na maisha ya kiroho, ndiyo maana anataka kuwatangazia kwamba, Yesu ni Bwana, kwa kuendelea kuimarisha mizizi ya imani iliyopandikizwa na waamini kutoka Korea. Wazee ni vyombo vinavyohifadhi hazina kubwa na vijana ni kielelezo cha hija ya watu.

Kanisa ni kielelezo cha Familia kubwa, mahali ambamo watu wanajisikia kuwa ni ndugu wamoja katika Kristo. Kwa jina la Kristo, Baba Mtakatifu anasema anakwenda nchini Korea ili kuwashirikisha Injili ya Upendo na Matumaini.







All the contents on this site are copyrighted ©.