2014-08-11 11:15:42

Papa Francisko anaguswa na mateso ya wananchi wa Iraq


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 10 Agosti 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro alitangaza kwamba, amemteua Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la uinjilishaji wa watu kumwalikisha rasmi nchini Iraq, kama kielelezo cha mshikamano wa dhati na wananchi wa Iraq ambao kwa sasa wanakabiliwa na majanga makubwa!

Baba Mtakatifu Jumapili jioni alikutana na kuzungumza na Kardinali Filoni kuhusu undani wa ziara yake nchini Iraq. Baba Mtakatifu ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na mateso na mahangaiko ya wananchi wa Iraq. Ametoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Iraq ambao kwa sasa wanakabiliwa na mahitaji makubwa, kama kielelezo makini cha mshikamano wake na Jumuiya ya Kimataifa inayoendelea pia kutoa msaada wa hali na mali.

Kardinali Filoni katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Vatican kabla ya kuondoka mjini Vatican siku ya Jumatatu kuelekea Iraq anasema kwamba, Baba Mtakatifu ameguswa sana na mahangaiko ya wananchi wa Iraq, pengine alitamani kuwepo mwenyewe ili kuonesha mshikamano wake, lakini dhamana hii amempatia Kardinali Filoni. Watu wanaoteseka na kuhangaika ndio maskini wa nyakati hizi wanaopaswa kuhudumiwa kikamilifu.

Kardinali Filoni anasema, utume wake nchini Iraq inapania kuwatia shime, imani na matumaini, ili kwamba, licha ya mateso na madhulumu wanayokabiliana nayo wasikate tamaa bado waendelee kutambua kwamba, Iraq ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa ambao kwa miaka mingi umewasaidia wananchi wa dini mbali mbali kuishi kwa amani na utulivu. Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya watu wanataka kuupoteza utajiri huu.

Hii ni hija ta matumaini kwamba, bado kuna matumaini ya kesho iliyo bora zaidi na kwamba, Kanisa la Kiulimwengu liko pamoja nao. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasaidia wananchi wa Iraq.







All the contents on this site are copyrighted ©.