Licha ya mawimbi mazito, lakini imani kwa Kristo inaweza kuwaokoa waja wake!
Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa tafakari yake ya Injili ya Jumapili ya kumi na
tisa ya kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican, Jumapili tarehe 10 Agosti 2014 amefafanua kuhusu muujiza wa Yesu kutembea
juu ya bahari baada ya kufanya muujiza wa kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano
na samaki wawili.
Mitume walipomwona Yesu anatembea juu ya bahari walishikwa
na woga, lakini Yesu mwenyewe aliwatuliza. Kama ilivyo kawaida ya Mtakatifu Petro,
akataka kuhakikisha kweli kwamba, alikuwa ni Yesu, akamwomba ili yeye pia aweze kutembea
juu ya bahari. Yesu akamkaribisha na Petro akaanza kutembea juu ya bahari, lakini
alipoona upepo mkali akaanza kuzama na hatimaye akampigia kelele Yesu ili aweze kumwokoa.
Papa
Francisko anasema, Mtakatifu Petro aliitambua sauti ya Kristo, akajiachilia mikononi
mwa Yesu ambaye ni Mwalimu na Bwana akamfuata. Mtakatifu Petro alianza kuzama pale
alipoonesha mashaka, lakini Yesu yuko daima tayari kuwaokoa wale wanaomkimbilia.
Huyu
ndiye Mtume Petro anayeonesha ukakamavu na mapungufu yake, kielelezo cha imani ya
Wakristo ambayo daima inaonesha umaskini, lakini yenye nguvu ya kupata ushindi; hii
ni imani ya Mkristo anayetembea ili kukutana na Yesu Kristo mfufuka, kati ya mawimbi
mazito na hatari za maisha.
Baba Mtakatifu anasema, Yesu alipopanda kwenye
mashua mambo yote yakawa shwari, kiasi cha Mitume wote kumwabudu Yesu kuwa ni Mwana
wa Mungu. Ndani ya mashua kuna Mitume wenye uzoefu na mang'amuzi ya mapungufu yao
ya kibinadamu, wasi wasi na mashaka, lakini kwa pamoja wanajisikia wamoja katika imani
wakimzunguka Yesu Kristo. Bila kuwa karibu na Yesu, daima wafuasi wake watajisikia
waoga, kwani hiki ni kielelezo cha ukosefu wa imani, lakini Yesu yuko tayari kuwaokoa
waja wake wanapomlilia kwa imani na matumaini.
Hii ndiyo sura ya Kanisa ambalo
halina budi kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha, lakini waamini wanaweza
kuokolewa ikiwa tu watakuwa na imani thabiti, inayowawezesha kutembea hata katika
giza na uvuli wa mauti bila ya kuogopa. Imani inawahakikishia waamini uwepo endelevu
wa Kristo katika maisha yao. Waamini wanaweza kujisikia kuwa salama pale tu wanapopiga
magoti ili kumwabudu Mwana wa Mungu.