2014-08-11 08:57:17

Imani haina budi kumwilishwa katika matendo ya kila siku, ili kuyachachua malimwengu!


Kanisa linaonesha uhai pale linaposhikamana na Mwenyezi Mungu na kumjali mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu katika mahitaji yake yote: kiroho na kimwili, vinginevyo, Kanisa linaonesha dalili za kuchoka na hatima yake ni kifo.

Uhai wa Kanisa unajionesha katika maisha na utume wake unaojikita katika: Imani, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, Maisha adili yanayoongozwa na Amri za Mungu pamoja na maisha ya Sala, kama kielelezo cha majadiliano ya kina kati ya Mungu na mwanadamu. Imani haina budi kumwilishwa katika matendo ya kila siku, ili kuyachachua malimwengu kwa harufu ya utakatifu wa maisha. Waamini wengi wana ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Kwa ufupi haya ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anazungumza moja kwa moja na Kituo cha Radio cha Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, iliyoko Kaskazini mwa Argentina. Baba Mtakatifu anasema, waamini si watoto yatima kwani wanaye Mama na mwombezi ambaye ni Bikira Maria anayewafariji na kuwapatia changamoto yakufarijiana wao kwa wao. Kanisa halina budi kujikita katika maisha ya: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza waamini wote wanaojikita katika mtazamo kama huu wa maisha yao ya Kikristo, kwani kwa njia hii, wanayatakatifuza malimwengu. Anawapongeza waamini wanaosaidia kwa hali na mali katika maisha na utume wa Kanisa, lakini mali na utajiri visiwe ni sababu ya kinzani na migawanyiko ya kijamii. Mama Kanisa hana budi kuendeleza hija ya maisha yake hapa duniani, ili kujenga na kuimarisha Ufalme wa Mungu pasi na kuchoka.

Hija hii ijikite katika undani wa maisha ya waamini, kwa kumwamini, kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Ni hija inayopania kuwasaidia jirani katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili. Hija hii ya maisha ni endelevu na kamwe haina ukomo, hadi pale mwamini atakapokutana na Muumba wake uso kwa uso. Waamini wafanye hija kwa njia ya Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kuachana kabisa na “tabia ya majungu kwani hayana mtaji, kama kweli yangekuwa ni mtaji, watu wengi wangetajirika”, lakini majungu yanasababisha kinzani, majeraha ndani ya Jumuiya. Watu wajielekeze zaidi katika ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati kwani tofauti kati ya watu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Pale kinzani na migongano inapojitokeza, watu waoneshe ukomavu wa kukaa chini na kuanza kujadiliana katika ukweli, uwazi, daima wakitafuta mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana wa kizazi kipya kuonesha ujasiri wa kufanya maamuzi magumu pale Mwenyezi Mungu anapobisha hodi katika milango ya mioyo yao akiwataka kujisadaka kwa ajili ya Kanisa na Jirani zao katika maisha na utume wa Kipadre na Kitawa. Vijana wasiwe na woga bali watambue kwamba, Yesu anataka kuwashirikisha katika utume wake wa kuwafariji na kuwatangazia watu Injili ya Furaha.

Kwa wale wanaojisikia kwamba, wito wao ni maisha ya ndoa na familia, waendeleze dhana hii kwa kujenga familia ya Kikristo, ambayo kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani. Watambue kwamba, Mungu ni upendo na kamwe hachoki kuwamegea waja wake upendo, huruma na msamaha.

Baba Mtakatifu amewabariki wote waliokuwa wanamsikiliza moja kwa moja kutoka mjini Vatican anawatakia nguvu ya kusonga mbele pasi na kukata tamaa, ujasiri wa kushikamana na Kristo pasi ya kuwaruhusu baadhi ya watu kuwapokonya matumaini waliyo nayo, lakini zaidi, anawatakia amani na furaha ya ndani, inayojionesha kwa tabasamu la nguvu!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.