2014-08-11 08:47:36

Fadhila ya uvumilivu!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Kwa mara nyingine tena karibu katika kipindi chetu, tuendelee kuitazama familia kama shule ya fadhila mbalimbali. RealAudioMP3

Baada ya kuitazama fadhila ya unyenyekevu na umuhimu wake, na kisha kuona kilema pinzani cha unyenyekevu ambacho ni kiburi; leo tuendelee kwa kuitazama fadhila ya uvumilivu. Fadhila ya uvumilivu kwa mazingira fulani huambatana pia na saburi.

Tafakari hii inaongozwa na neno la Mungu lisemalo “mwanangu, ukienda kumtumikia Bwana, uwe tayari kupata majaribu. Uwe na moyo mnyoofu na nia moja; na usihangaike wakati wa taabu...uyapokee yote yatakayokupata hata ukiaibishwa, uwe na uvumilivu...mtegemee Mungu naye atakusaidia, shika njia nyoofu na kumtumaini yeye” (rej. YbS 2:1-6)
Uvumilivu ni nini?

Uvumilivu ni hali ya kustahimili magumu au mapungufu fulani ya maisha. Ule ustahimilivu katika saburi ndiyo huitwa uvumilivu. Tunakubaliana kwamba katika maisha yetu ya kila siku tunapatwa na magumu mbalimbali. Na sio kila gumu linalotujia tunaweza kulitatua kwa muda huu. Yapo baadhi ya magumu ambayo tunaweza kuyatatua kwa akili zetu na kwa msaada wa wenzetu, na yapo mengine hatuwezi kuyatatua kabisa. Yapo yale ambayo hatuwezi kuyatatua kwa sasa, lakini baada ya muda fulani tutaweza kuyatatua. Ni katika hayo ambayo hatuwezi kuyatatua kwa sasa, ndiyo yahitaji uvumilivu, ustahimilivu, saburi.

Fadhila hii inatusaidia kuzuia au kuondoa mahangaiko yasiyokuwa ya lazima pale tunapotatika. Pasipo ustahimilivu na saburi, hutokea kwamba tunahamaki kupita kiasi pale tunapopatwa na tatizo. Tunahamaki kiasi cha kuyatatiza matatizo tunayokuwa nayo. Twaweza kuwa tulipatwa na tatizo dogo sana, lakini kwa vile tulihamaki, hatukua na uvumilivu, papara zetu zimetufanya tulikuze tatizo kupita kiasi hadi linashindwa kutatulika tena.

Kukosa uvumilivu yaweza kuwa ni tabia kwa baadhi ya watu. Wao wakajenga fikra kwamba kila kitu lazima kipatikane sasa, kila tatizo lazima litatuliwe sasa, kila ombi lazima lijibiwe sasa. Na wanapokosa wanayoyataka kwa muda wanaoutaka wao, basi hapo huzua fujo. Maisha hayaendi hivyo, tunahitaji kuwa na saburi ya kutosha katika maisha. Tukilazimisha mambo kwa namna tunavyotaka na kwa wakati tunaotaka, kuna hatari ya kutumia hata mbinu za dhambi ili kufanikisha mambo yetu.
Aina mbalimbali za uvumilivu:

Uvumilivu wa kimwili na kiakili:- hii ni saburi inayohitajika pale ambapo tunakuwa na mahitaji ya kimwili, tunapopatwa na magonjwa, tunapopatwa na mahangaiko ya kijamii kama vile mahusiano yetu yanapoingia dosari, tunapokosa kueleweka vizuri na wenzetu na pale ambapo mifumo ya kijamii haiendi vizuri. Tunachohitaji ni uvumilivu katika saburi, huku akili tulivu ikitafuta njia sahihi ya kutuondoa katika adha hizo. Katika adha za kimwili na kijamii tunapokosa saburi, ndipo hapo zinapozuka fujo na migomo-haribifu. Ni katika uvumilivu na saburi tunaweza kuteti katika meza ya mviringo na kutafuta suluhu sahihi la matatizo yetu.

Uvumilivu wa kiroho:- huu huhitajika katika mambo yote ya kiroho. Sisi tunaomwamini Mungu mara nyingi kwa imani tunamtolea Mungu sala na maombi yetu. Ni katika uvumilivu tunasubiria huruma ya Mungu. haimaanishi kwamba tumemwambia Mungu shida zetu na saa hiyo hiyo lazima atoe jibu, hasha!! Tunamwekea Mungu matumaini yetu, tunangojea kwa matumaini kutimiziwa huruma yake. Saburi ya kiroho hutualika daima kutafuta muungano na Mungu na kusubiria ahadi zake. Tunapomwomba Mungu jambo, basi tusubiri huruma yake katika hali ya sala, huku tukijibidisha kutenda kile tuwezacho kwa maweza yetu.

Fadhila ya uvumilivu wenye utulivu na saburi, isaidie katika jamii zetu kuzuia fujo za mara kwa mara, ambazo kimsingi si shida ni watu kukosa uvumilivu na saburi. Familia zetu ziwafundishe watoto uvumilivu na saburi kwa maneno na matendo. Watoto wakizoeshwa kuvumilia kero mbalimbali kwa saburi, hakika katika ule umri wa fujo na ukubwani, hawataleta migomo ya mashinikizo kutaka kila tatizo lao litatuliwe hapohapo.

Mpendwa msikilizaji, uvumilivu husaidia kuleta amani katika jamii ya watu. Sisi sote tujijenge katika uvumilivu. Na kwa wale wenye dhamana ya utumishi juu ya watu, wasiudharau uvumilivu wa watu. Uvumilivu ni kwa ajili ya kusaidia kupata hali njema, na siyo kwa ajili ya kuendelea kuteseka. Tusikilizane tena kipindi kijacho.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.