2014-08-11 12:00:08

Dunia inawahitaji vijana jasiri!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili asubuhi tarehe 10 Agosti 2014 amezungumza kwa simu moja kwa moja na vijana wa Skauti waliokuwa wamekusanayika huko San Rossore, mjini Pisa, Kaskazini mwa Italia ili kuhitimisha safari ya tatu kitaifa ya Skauti, AGESCI, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu "Njia ya ujasiri, kuelekea siku za usoni". Baba Mtakatifu amefanya mazungumzo haya na vijana wa Skauti mara tu baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Baba Mtakatifu anasema, anawasikindikiza katika hija yao kwa njia ya sala na kwamba hija wanayoifanya ni kwa ajili ya mafao yao kwa siku za usoni, kwa kujikita katika fadhila ya ujasiri karama kwa maisha ya vijana. Dunia inawahitaji vijana wajasiri na wala si waoga; vijana ambao wako tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini bila kujikatia tamaa, kwani inasikitisha kumwona kijana amezeeka hata kabla ya wakati wake.

Ujasiri miongoni mwa vijana utazaa matunda kwa wakati wake na hiki ni kielelezo cha ushindi, katika mchakato wa kuleta mabadiliko, ili kweli ulimwengu uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kujikita katika ukweli, utashi mwema na uzuri unaobubujika kutoka kwa Kristo. Baba Mtakatifu anawataka vijana kutokuwa na woga na wala wasikubali kupokonywa matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Vijana waendelee kuwa na ujasiri!







All the contents on this site are copyrighted ©.