Mjumbe wa Baraza la Uendeshaji la UNESCO linalosimamia ukuzaji wa utamaduni, Dk. Mary
Mbiro Khimulu amesema machafuko na mauaji hayana uhusiano wowote na dini ambayo ni
ya kweli. Ametoa kauli hiyo Jumatatu, Agosti 11, 2014 wakati akishiriki mjadala wa
jinsi ambavyo Bara la Afrika linakabiliana na migogoro inayotokea barani humo kwenye
mkutano wa Dunia unaojadili masuala ya Amani, Usalama na Maendeleo jijini Seoul, Korea
ya Kusini.
Dk. Khimulu ambaye ni raia wa Kenya, alisema: "Dini ya kweli haiwezi
kuruhusu umwagaji wa damu, hakuna dini ya kweli inayochochea mauaji wala kuruhusu
mapigano. Ninawasihi wote mliopo hapa, msiruhusu dini zenu zitumike kufanya mambo
mabaya."
Dk. Khimulu alisema ili kuepuka migogoro ya dini, anashauri diplomasia
ya utamaduni (cultural diplomacy) itumike kuleta amani, usalama na maendeleo barani
Afrika. "Kwa kuitumia diplomasia ya utamaduni, tuangalie ni kwa njia gani mijumuiko
ya pamoja ya kidini (inter-faith communities) inaweza kutumika kuleta amani, upendo
na mshikamano kwenye jamii tunazoishi," alisema.
Vilevile, Dk. Khimulu alisema
kwa kutumia diplomasia ya utamaduni tunaweza kuvunja chuki na kuleta mshikamano na
umoja miongoni mwa watu wetu, watu wakatembeleana kupitia michezo, nyimbo au matamasha,
na wakajenga mahusiano ya kuheshimiana kidugu.
Alisema kwa kuwa vita huanzia
akilini mwa mwanadamu, ni humo humo ambamo mawazo ya kuacha mapigano ama machafuko
yanapaswa kuingizwa. "Kwa hiyo tuitumie diplomasia ya utamaduni kama njia pekee ya
kujenga mahusiano ya karibu kwenye jamii zetu na itusaidie kufikia malengo yetu ya
kupata amani na usalama kwa watu wetu,"aliongeza.
Mapema, Balozi wa Kudumu
wa Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Antonio Tete alisema wakati Umoja
wa Afrika unaanzishwa mwaka 1963, baadhi ya wakuu wa nchi walikuwa na ndoto ya kuwa
na jeshi moja barani Afrika ambalo lingekuwa na kazi ya kukabili migogoro yote barani
humo.
"Kutokana na mabadiliko ya wakati na kadri muda ulivyosonga mbele, matarajio
yao hayakutumia. Viliundwa vikosi vya muda navyo havikudumu. Tumeshuhudia miaka ya
90 kwenye migogoro ya Rwanda na ya Somalia. Hakuna jeshi lilipelekwa wala hakuna askari
waliokuja kutoka nje," alisema.
Alisema Umoja wa Afrika unakabiliwa na changamoto
ya kukosa fedha za kujiendesha kubwa likiwa ni la kusimamia amani na usalama wa nchi
wanachama. “Tunayo programu ya ulinzi na usalama lakini asilimia 90 ya mpango huu
inachangiwa na wafadhili kutoka nje ya nchi. Hii siyo kazi rahisi... huwezi kujiendesha
namna hii,” alisema.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni kuwepo kwa vikund vya
kigaidi. “Hawa wanaendesha mambo yao tofauti na kwa teknolojia ya hali ya juu, hata
ungekuwa na jeshi la aina gani si rahisi kuwashinda... huwezi kutumia njia za kawaida
za kupambana na uhalifu unapokabiliana na makundi ya aina hii,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Balozi Tete aliwaomba baadhi ya washiriki wafikirie kuwekeza Barani
Afrika kama njia mojawapo ya kuleta amani ya kudumu katika bara hilo. “Kwa muda mrefu
bara hili limetumika kama chanzo cha malighafi kwa viwanda vya Ulaya na Amerika. Ni
wakati sasa tubadili muelekeo na tufikirie kuwekeza katika bara hili kwani kwa kufanya
hivyo mtasaidia kutengeneza ajira nyingi kwa vijana wa Afrika kupitia viwanda ambavyo
mtavijenga.”
“Kukiwa na ajira za kutosha, mtaleta maendeleo na mtaleta amani
kwa vile mtapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro na machafuko yanayotokana na kugombea
rasilmali haba zilizopo,” alisema.