2014-08-09 09:10:25

Mchango wa Kanisa Katoliki Tanzania katika sekta ya elimu!


Askofu John Ndimbo, Mwenyekiti wa Idara ya Elimu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio vatican anabainisha mchango wa Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo, ili kuhakikisha kwamba, elimu inasaidia kumpatia mwanadamu ukombozi wa kweli, kiroho na kimwili, kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa utume ulioanzishwa na Yesu, Mwalimu na Mponyaji! RealAudioMP3

Kanisa Katoliki Tanzania kwa sasa linaundwa na majimbo 34 na walau kila Parokia imebahatika kuwa na shule ya awali na kwamba, Kanisa linamiliki na kuendesha shule za msingi 100, Sekondari 220, zikiwemo Seminari 37 kwa ajili ya majiundo makini ya Makasisi kwa siku za usoni. Shule hizi zinamilikiwa na kuendeshwa na Majimbo pamoja na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yanayotekeleza dhamana na wajibu wake nchini Tanzania.

Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendesha vyuo vya ufundi stadi 75 ambavyo vimesajiliwa na VETA. Hapa wanafunzi ambao hawakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari wanapatiwa mafunzo ya taaluma, ili kuweza kujiajiri mara tu wanapohitimu masomo yao. Kanisa pia linamiliki na kuendesha vyuo vikuu viwili: Chuo kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania, SAUT pamoja na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Mwambata, Bugando, CUHAS, bila kusahau matawi ya vyuo kumi ya vyuo hivi yaliyoenea sehemu mbali mbali za Tanzania.

Askofu Ndimbo anasema kwamba, Kanisa Katoliki Tanzania limepata mafanikio makubwa kwenye sekta ya elimu kutokana na ubora, umakini wa elimu inayotolewa katika vyuo vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki kwa kuzingatia viwango vya elimu. Matunda yake yanaonekana katika soko la ajira ndani na nje ya Tanzania.

Pamoja na mafanikio yote haya, Askofu Ndimbo kwa unyenyekevu mkubwa anakiri kwamba, taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki Tanzania bado zina uwezo mdogo ikilinganishwa na hitaji la wanafunzi wanaoomba kujiunga na vyuo hivi. Baadhi ya shule zinatoza ada kubwa na hivyo familia za maskini na watu wa kawaida wanashindwa kufaidika na huduma ya elimu inayotolewa na Kanisa.

Kuna mwelekeo mkubwa kwa mashirika mengi ya kitawa kutaka kujenga shule na taasisi za elimu mijini, hali inayoonesha kwamba, kama hakuna mikakati ya makusudi, huduma ya elimu inayotolewa na Kanisa Katoliki vijijini inaweza kuathirika vibaya, hapa kinachotafutwa ni soko!

Askofu Ndimbo anasema, Kanisa bado linakabiliwa na uhaba wa nguvu kazi na rasilimali watu ili kuendesha taasisi za elimu nchini Tanzania na kwamba, bado kuna taasisi za elimu zinazoendeshwa kimapokeo, mwelekeo ambao umepitwa na wakati, kiasi cha kusababisha weledi kuwa hafifu, kuna haja kwa Kanisa kuwekeza katika majiundo ya rasilimali watu, ili kuendeleza mbele mafanikio yaliyokwishakupatikana katika sekta ya elimu nchini Tanzania. Kuna haja pia ya kuwa na uhakika wa rasilimali fedha kwa kujijengea misingi ya kujitegemea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.