2014-08-09 11:28:50

Korea ya Kusini inaendelea kuwekeza katika majadiliano ya kiekumene!


Kuanzishwa kwa Tume ya Kiekumene ya Imani na Katiba kunako tarehe 22 Mei 2014 nchini Korea ya Kusini imekuwa ni hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa nchini humo. Haya ni matunda ya ushirikiano wa miaka mingi baina ya Makanisa na kwamba, kwa sasa wanasubiri kwa hamu kubwa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko, ili kuvuka vikwazo vilivyopitwa na wakati tayari kuanza mwelekeo mpya wa majadiliano ya kiekumene.

Kanisa Katoliki nchini Korea ya Kusini linapenda kujielekeza zaidi na zaidi katika kukuza na kuimarisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa, haki na amani mintarafu utangazaji wa Injili ya Furaha unaohimizwa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya ushiriki wa azma ya Uinjilishaji Mpya. Huu ni ushuhuda wa imani tendaji unaojionesha katika uhalisia wa maisha ya waamini kila siku nchini Korea ya Kusini. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni nyenzo msingi hata katika kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Karne ya ishirini imeacha madonda na mahangaiko makubwa kwa wanachi wa Korea kutokana na vita iliyopelekea mgawanyiko wa Korea mbili bila kusahau majanga yaliyosabishwa na vita hii, ambayo kamwe haitasahaulika miongoni mwa wananchi wa Korea, kwani hadi leo hii kuna hatari kwamba, Nchi hizi mbili ambazo kimsingi ni pacha zinaweza siku moja kupimana nguvu kwa njia ya mtutu wa bunduki.

Katika kipindi chote hiki, Wakristo na Waamini wa dini mbali mbali nchini humo kwa njia ya majadiliano ya kiekumene na kidini wamejitahidi kupandikiza mbegu ya msingi wa haki, amani; kwa kukazia haki msingi za binadamu. Tangu mwaka 1924 hadi leo hii, Korea imepiga hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Wataalam wa majadiliano ya kiekumene wanasema, kuna haja kwa Makanisa kuendelea kuwekeza katika majiundo makini ya kiekumene, ili Wakristo kwa pamoja waweze kutolea ushuhuda wao amini kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini hawana budu kuachana na falsafa ya kutumia nguvu na badala yake waunganishe nguvu zao katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na utulivu.







All the contents on this site are copyrighted ©.