2014-08-08 10:03:44

Marekani kuwekeza katika masuala ya ulinzi na usalama Barani Afrika!


Rais Barack Obama wa Marekani katika mkutano na wakuu wa Serikali kutoka Barani Afrika amesema kwamba, Marekani itachangia kiasi cha dolla za kimarekani millioni mia moja na kumi katika kipindi cha miaka mitano, ili kuimarisha amani, ulinzi na usalama Barani Afrika.

Fedha hii itaelekezwa zaidi nchini Senegal, Ghana, Ethiopia, Rwanda, Tanzania na Uganda. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanajeshi katika vikosi vya ulinzi na usalama vya Umoja wa Afrika wanahatarisha sana maisha yao wakati wakitoa huduma ya ulinzi na usalama, kumbe anasema Rais Obama, Marekani inapenda kuimarisha mchakato wa ulinzi na usalama Barani Afrika, ili kukabiliana na changamoto za vitisho kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano na viongozi wakuu wa Serikali kutoka Barani Afrika, Rais Obama ameonesha kuridhishwa na mkutano wa siku tatu ambao ni wa aina yeka kuwahi kuitishwa na Serikali ya Marekani. Ulinzi na usalama, fursa za ajira pamoja na utawala bora ni kati ya mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee katika mkutano huu. Marekani inataka kuwekeza katika ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.