Changamoto katika utoaji wa huduma za kijamii nchini Tanzania
Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge - Ngara ambaye pia ni Makamu
wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican
anabainisha kwamba, huduma za kijamii zinazotolewa na Kanisa ni sehemu ya mchakato
wake wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Lakini ikumbukwe
kwamba, serikali inawajibika kutoka huduma za kijamii kwa ajili ya watu wake. Kumbe,
Kanisa linachangia katika maboresho ya huduma za kijamii nchini Tanzania. Ili kutekeleza
azma hii kuna haja ya kuimarisha ushirikiano zaidi kati ya Kanisa na Serikali. Dhana
ya kwamba, Kanisa linafaidika sana kutokana na huduma inazotoa katika sekta ya jamii
ni kikwazo kikubwa cha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa katika kuwahudumia watanzania.
Askofu
Niwemugizi anasema kwamba, Kanisa inakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwepo uhaba
wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeshea taasisi zake za afya. Hapa Serikali katika
sera yake ya ushirikiano na taasisi binafsi ilikwisha sema kwamba, itasaidia kulipia
mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya afya wenye taaluma na viwango vinavyotakiwa,
lakini hata hili utekelezaji wake bado unasuasua kwa kiasi kikubwa!
Askofu
Niwemugizi anabainisha kwamba, Makanisa na Halmashauri yalianza mchakatato wa majaribio
ya mikataba mipya, lakini hata hapa bado utekelezaji wake bado ni kidogo sana, kiasi
cha kukwamisha jitihada za Kanisa katika kushiriki kwenye mchakato wa maboresho ya
maisha ya watanzania kwa kuchangia katika utoaji wa huduma za kijamii.