Mshikamano wa Papa na wananchi wa China waliokumbwa na tetemeko la ardhi!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kwa mahujaji na wageni waliokuwa
wamefurika mjini Vatican, Jumatano tarehe 7 Agosti, 2014, amewakumbuka na kuonesha
mshikamano wake wa pekee kwa wananchi wa China waliokumbwa na tetemeko la ardhi ambalo
hadi sasa limekwishasababisha maafa makubwa.
Taarifa zilizotolewa na Serikali,
Alhamisi tarehe 7 Agosti 2014 zinaonesha kwamba, watu 589 wamefariki dunia, watu
9 hawajulikani mahali waliko na wengine 2, 401 wamepata majeraha makubwa. Serikali
ya China imelazimika kuwahamisha wananchi 230, 000 kutoka katika makazi yao, ili kuwapatia
hifadhi mahali pa salama zaidi.
Baba Mtakatifu anawaombea marehemu waliopoteza
maisha yao kwenye Jimbo la Yunnan na anawakumbuka katika sala zake, wote waliokumbwa
na janga hili. Baba Mtakatifu katika tafakari yake kwa lugha ya kiarabu amewakumbuka
na kuwaombea pia wananchi wa Iraq ambao kwa sasa wanateseka kutokana na vita kupamba
moto hasa eneo la Kaskazini mwa Iraq. Anawaombea ili amani ya kweli iweze kupatikana!