2014-08-07 12:19:52

Marekani imeamua kuwekeza kweli Barani Afrika!


Rais Barack Obama wa Marekani katika mkutano na viongozi wakuu wa Serikali Barani Afrika uliokuwa unafanyika mjini Washington DC, amesema kwamba, Serikali yake itawekeza kiasi cha dolla za kimarekani billioni thelathini na tatu, kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake wakati alipotembelea Barani Afrika, mwaka 2013.

Katika mkutano ambao umehitimishwa rasmi siku ya jumatano tarehe 6 Agosti 2014 imekuwa ni fursa makini kwa Marekani kubainisha mikakati yake ya kiuchumi kama kielelezo cha mshikamano wa dhati katika kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi Barani Afrika. Licha ya changamoto zote hizi, Bara la Afrika linaanza kupata mwelekeo mpya na kwamba, Serikali ya Marekani inapenda kuwa ni mdau mkubwa katika mchakato wa maendeleo Barani Afrika.

Rais Obama anasema, ili kuwekeza Barani Afrika kuna haja kwanza kabisa kuhakikisha kwamba, kuna amani na utulivu. Makampuni makubwa yapatayo kumi na manne kutoka Marekani yatawekeza kiasi cha dolla billioni kumi na nne katika masuala ya ujenzi, nishati rafiki, huduma za kibenki na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kiasi cha dolla za kimarekani billioni kumi na mbili kitatumika kwa ajili ya kuendeleza nishati Barani Afrika, mkakati unaotekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na sekta binafsi. Serikali ya Marekani inatarajia kutoa kiasi cha dolla za kimarekani billioni saba kwa ajili ya maboresho ya biashara ya nje. Mikakati yote hii inalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Bara la Afrika, kwa kuongeza pia fursa za ajira na ukuaji wa uchumi Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.