Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa lapata "Majembe mapya"
Askofu Emmanuel Barbara wa Jimbo Katoliki Malindi ambaye pia ni msimamizi wa kitume
wa Jimbo kuu la Mombasa, katika Ibada ya Misa Takatifu kabla ya uchaguzi mkuu wa Shirika
la Masista wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa, amewaambia Watawa hao kwamba,
Mwenyezi Mungu huchagua viongozi sio kwa sababu ya uwezo wao wa kiakili au nguvu walizo
nazo, bali ni kwa sababu anataka kuwaimarisha na kuwatumia kama vyombo vya kueneza
utukufu wake.
Viongozi wanaochaguliwa kuwaongoza watawa wenzao wanakumbushwa
kwamba, wanaitwa kuwa wahudumu, wanaopaswa kusaidiana kwa kuoshana miguu kama alivyofanya
Yesu mwenyewe kwa wanafunzi wake. Hii ni changamoto ya kutoa huduma makini na yenye
tija kwa Watu wa Mungu bila kubagua, kama anavyojitahidi kufanya Baba Mtakatifu Francisko
katika maisha na utume wake. Viongozi wawe ni mfano wa unyenyekevu, walezi wema,
wapole na watakatifu, ili kuwasaidia watawa wenzao kuishi kweli za Kiinjili kwa kuendeleza
maisha ya kitawa, tayari kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Wajumbe
wa mkutano mkuu wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa wamemchagua
Sr. Jane Irene Awuor kuwa Mama mkuu wa Shirika na Msaidizi wake ni Sr. Elizabeth
Nduku. Washauri wakuu wa Shirika ni Sr. Terezia Waweru, Sr. Betty Shao pamoja na Sr.
Bridgita Mwawasi.
Askofu Emmanuel Barbara amewataka viongozi wapya kutekeleza
dhamana na wajibu wao kikamilifu wakitambua kwamba, wanafanya dhamana hii kwa niaba
ya Shirika. Kumbe, wanapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwaongoza daima,
kama alivyofanya kwa Waisraeli walipokuwa wanaelekea kwenye Nchi ya ahadi, iliyojaa
maziwa na asali.
Askofu Barbara amewashukuru watawa kwa huduma bora wanazotoa
kwa ajili ya Familia ya Mungu ndani na nje ya Bara la Afrika, hasa kwa kuwahudumia
maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Masista hawa wameombwa kumwangalia
Mtakatifu Yosefu, aliyeonesha utii na unyenyekevu katika kutekeleza mpango wa Mungu
katika maisha yake, akawa Baba mlishi na mwema kwa Mtoto Yesu. Huu ni mwaliko kwa
Watawa kuandamana na Yesu katika kutangaza Injili ya Furaha kwani Yeye ndiye sababu
ya wito na maisha yao ya kitawa!